Motsepe aibeba Tanzania AFCON 2027
Muktasari:
- Kauli hiyo ya Motsepe inakuja wakati ikisalia miezi tisa kabla ya kufanyika kwa fainali hizo Juni 19, 2027 hadi Julai 17, 2027 ambapo hapa nchini vitatumika viwanja vitatu vya Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Uwanja wa Samia Suluhu Hassan (Arusha) na Fumba (Zanzibar).
RAIS wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Dk Patrice Motsepe, amekoleza wino kwamba bado ana imani na Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2027) kufanyika Afrika Mashariki katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.
Kauli hiyo ya Motsepe inakuja wakati ikisalia miezi tisa kabla ya kufanyika kwa fainali hizo Juni 19, 2027 hadi Julai 17, 2027 ambapo hapa nchini vitatumika viwanja vitatu vya Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Uwanja wa Samia Suluhu Hassan (Arusha) na Fumba (Zanzibar).
Akizungumza jana mara baada ya ziara yake hapa nchini, Motsepe alisema hakuna mpango B wala C kwenye wenyeji wa Fainali hizo za 2027 na kwamba CAF bado lina imani na maendeleo yanayofanyika Tanzania, Kenya na Uganda.
Motsepe alisema ingawa bado kuna maeneo yanahitaji kuboresha huku akigoma kuyataja, lakini imani yake inatokana na nguvu ambayo inawekwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pamoja na Serikali katika maandalizi hayo.
"Nimekuja kuangalia namna kazi inavyoendelea katika uwanja huu wa Mkapa, unajua mimi nina imani kubwa na uwanja huu hata wakati tunataka kufanya uamuzi wa uwanja upi utumike kwenye fainali ya Shirikisho kati ya Simba na Berkane, nilisema wazi kwamba napenda ifanyike hapa," alisema Motsepe.
"Naona kazi inaendelea, nataka niiambie Afrika na wanachama wetu kwamba, hakuna mpango B wala C, CAF bado ina imani na kazi kubwa inayoendelea hapa, nilikuwa hapa Februari lakini naona kuna mabadiliko yanayotia moyo.
"Kuna changamoto chache ambazo naamini kwa nguvu ambayo inafanywa na serikali ya Tanzania pamoja na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania, Wallace Karia tutafikia malengo yetu, CAF tutakuwa pamoja nao."
Aidha, Motsepe aliongeza kuwa, ziara yake ijayo itafanyika Januari 2027 ambapo anaamini mpaka kufikia hapo mambo yote muhimu yatakuwa yamefikia pazuri tayari kwa mashindano hayo makubwa.
"Tumesalia na miezi tisa mpaka kufanyika kwa fainali hizi, ziara yangu ijayo na ya mwisho nitakuja hapa Januari mwakani, naipongeza sana serikali ya Tanzania lakini mpaka kufikia hapo naamini tutakuwa tumepiga hatua kubwa kwenye kazi hii.
"Leo (jana mchana) nitaonana na Waziri Mkuu (Dk Mwigulu Nchemba), nitakuwa na kikao naye lakini nikitoka hapa leo (jana) Tanzania nitakwenda Kenya kuonana na Rais William Ruto, bahati mbaya sitakwenda Uganda kutokana na masharti ya ugonjwa wa Ebola.
"Nitakuwa na mkutano nchini Marekani na nitatakiwa kuwa kwenye uangalizi wa siku 21 kabla ya kuingia Marekani kama nitatokea Uganda, kwa hiyo Uganda nitakwenda baadaye kwa ziara maalumu kuonana na Rais Yoweri Museveni."
Katika ziara hiyo ya Motsepe aliambatana na Makamu wake wa pili, Kurt Orkaku, kaimu katibu mkuu wa CAF, Samson Adamu Feizal Sidat na Rais wa Umoja wa Klabu Afrika (ACA), Hersi Said ambapo wote wakiwa na mwenyeji wao Wallace Karia na Naibu Waziri wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Khamis Mwinjuma walitembelea sehemu mbalimbali za Uwanja wa Mkapa.
Maeneo ambayo Motsepe alipitishwa baada ya kikao na naibu waziri ni pale wanapokaa wageni mashuhuri maarufu VVIP, sehemu ya kukaa waandishi wa habari, eneo la mkutano wa wanahabari huku pia akipata maelezo ya eneo la kuchezea.