Tanzania yaanza safari ya Woodball kimataifa
Muktasari:
- Ushiriki huo ni wa kwanza kwa Tanzania katika mashindano hayo, huku timu hiyo ikilenga kufanya vizuri na kupata nafasi ya kufuzu kushiriki mashindano ya dunia yatakayofanyika Taiwan, Desemba mwaka huu.
TIMU ya Taifa ya Woodball imeagwa rasmi kwenda Nairobi, Kenya, kushiriki Mashindano ya tisa ya Kimataifa ya Woodball Championship, yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Septemba 18 hadi 22, 2026 katika Chuo cha Mount University.
Ushiriki huo ni wa kwanza kwa Tanzania katika mashindano hayo, huku timu hiyo ikilenga kufanya vizuri na kupata nafasi ya kufuzu kushiriki mashindano ya dunia yatakayofanyika Taiwan, Desemba mwaka huu.
Mashindano hayo yanatarajiwa kushirikisha timu kutoka mataifa mbalimbali, yakiwamo Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Sudan Kusini, huku wenyeji Kenya wakiwa miongoni mwa timu zitakazokuwa katika kinyang’anyiro hicho.
Akizungumza Septemba 16, 2026 wakati wa hafla ya kuiaga timu hiyo na kukabidhiwa Bendera ya Taifa, Afisa Michezo Mwandamizi wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Charles Maguzu aliwataka wachezaji kwenda Kenya wakiwa na dhamira ya kuiletea nchi heshima.
Maguzu amesema kikosi hicho kina sura ya kitaifa kwa kuwa kimeundwa na wachezaji kutoka mikoa mbalimbali nchini, hivyo kinapaswa kutumia fursa hiyo kuonyesha umoja na uwezo wa Tanzania katika mchezo huo.
“Timu hii ni ya taifa kwa sababu mchanganyiko wenu umehusisha mikoa mbalimbali hapa nchini, sio Dar es Salaam tu kama tulivyozoea. Kuna kutoka Kigoma, Dodoma na mikoa mingine. Hii inaonyesha kabisa kwamba imejipanga kama nchi kwenda kupeperusha bendera yetu kule nchini Kenya,” amesema Maguzu.
Amesisitiza umuhimu wa nidhamu, uaminifu, uzalendo na moyo wa kujitolea kwa wachezaji wakati wote wa mashindano, akiwataka kuiga mfano wa timu nyingine za Taifa ambazo zimekuwa zikifanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.
“Nendeni mkacheze kwa uaminifu mkubwa, kwa uzalendo, kwa moyo wa kujitolea kwa hakika kwamba mnaletea heshima taifa letu. Kaigeni mifano ya timu zingine ambazo zinashiriki mashindano ya kimataifa na kufanya vizuri,” amesema.
Maguzu pia alitoa wito kwa Watanzania na wadau wa michezo kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuiwezesha timu za Taifa kupata rasilimali muhimu, ikiwamo fedha na vifaa vya michezo.
“Niwaombe sana Watanzania wapenda maendeleo, hususani maendeleo ya michezo mbalimbali hapa nchini, washirikiane na Serikali ili kuweza kusaidia timu zetu za Taifa ziweze kupata fedha za kutosha kwa ajili ya matumizi, lakini pia kupata vifaa vitakavyotumika,” amesema.
Mwenyekiti wa Chama cha Woodball Tanzania, Winjuka Makuza amesema ushiriki wa Tanzania katika mashindano hayo ni hatua muhimu kwa mchezo huo ambao unaendelea kukua nchini.
Alitoa shukrani kwa Serikali kwa kuendelea kushirikiana na chama hicho na kusaidia kufanikisha safari ya timu hiyo na hatua hiyo inaonyesha umuhimu unaotolewa kwa maendeleo ya Woodball nchini.