Usahihi: Stars ilitajwa kwa sababu za ‘kiufundi’
Kim Poulsen, raia wa Denmark ndiye aliyekuwa Kocha Mkuu wa Stars. Hivyo, uamuzi huo mgumu ulikuwa juu yake kwani alikuwa na nguvu ya kusema anamhitaji nani au hamtaki nani kwenye benchi lake.
Muktasari:
- Kwa utaratibu ambao Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) tumejiwekea, Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inawajibika kucheza mechi za kalenda hiyo.
MACHI 5 mwaka huu duniani kote zilichezwa mechi za kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Kwa utaratibu ambao Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) tumejiwekea, Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inawajibika kucheza mechi za kalenda hiyo.
Tangu tulipojiwekea utaratibu huo mara zote Taifa Stars imecheza mechi hizo. Ikikosekana huwa ni katika mazingira ambayo yapo nje ya uwezo wa TFF, kwani inaweza kukubaliana kucheza mechi na X lakini dakika ya mwisho timu hiyo ikaamua kubadili mpinzani.
Hivyo, Februari 25 mwaka huu TFF ilitangaza kikosi cha wachezaji 22 kuunda Taifa Stars kwa ajili ya mechi dhidi ya Namibia (Brave Warriors). Mechi hiyo ilichezwa Windhoek, Namibia na matokeo yakawa sare ya kufungana bao 1-1.
Sura mpya katika kikosi ilikuwa ni mchezaji mmoja tu, ingawa wapo wengine ambao hawakuwahi kuwemo katika Stars lakini walishaitwa Young Taifa Stars (Future Taifa Stars). Mchezaji huyo ni Athanas Mdamu kutoka Alliance ya Mwanza.
Wakati TFF inaingia katika mechi hiyo ilikuwa na mambo mawili ya kuzingatia. Ikumbukwe kuwa wakati ameingia madarakani, Rais Jamal Malinzi alisema utafanyika uamuzi mgumu kuhusu Benchi la Ufundi la Taifa Stars. Tena kauli hii aliitoa mbele ya waandishi wa habari.
Jambo la pili ni utaratibu wa kucheza mechi za kalenda za FIFA tuliojiwekea kama nilivyoeleza hapo juu, na tayari makubaliano yalishafanyika kati ya TFF na Chama cha Soka Namibia (NFA) juu ya mechi hiyo.
Ni dhahiri kuwa ukiambiwa uamuzi mgumu kuhusu benchi la ufundi, ni wazi uamuzi huo utamgusa moja kwa moja kiongozi wa benchi hilo. Itakuwa jambo la ajabu kudhani uamuzi huo ungemgusa kocha wa makipa au daktari wa timu na kumuacha Kocha Mkuu.
Kim Poulsen, raia wa Denmark ndiye aliyekuwa Kocha Mkuu wa Stars. Hivyo, uamuzi huo mgumu ulikuwa juu yake kwani alikuwa na nguvu ya kusema anamhitaji nani au hamtaki nani kwenye benchi lake.
Uamuzi kuhusu Poulsen tayari umefanyika kwa upande wake, na TFF kwa upande mwingine. Pande hizo zimekubaliana kuvunja mkataba kwa makubaliano yanayobakia kuwa siri kati yao.
Kikosi cha Stars kilichocheza na Namibia kilikuwa chini ya Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi ambaye ndiye aliyeteua wachezaji wale 22 walioikabili Namibia kule Windhoek.
Madadi ambaye ana leseni ya ukocha ya daraja A inayotambuliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) si mara yake ya kwanza kuifundisha Taifa Stars. Hivyo, uamuzi wa kumpa Stars kwa ajili ya mechi hiyo haukuwa wa bahati mbaya.
Kisheria isingekuwa sahihi Madadi kutangaza Taifa Stars wakati Kim Poulsen alikuwa bado ana mkataba wa kuinoa timu hiyo. Ndiyo maana TFF kupitia kwa Ofisa Habari wake ililazimika kufanya kazi hiyo ya kutaja kikosi ingawa aliyekiteua alikuwa ni Madadi.
Baadaye Madadi alitangazwa kuwa ndiye aliyeteua kikosi hicho na atakiongoza kwa mechi ya Namibia pekee. Wakati anatajwa tayari TFF na Kim Poulsen walishatangaza kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba. Kimsingi mkataba tayari ulikuwa umevunjwa.
Kama kuna mtu hataelewa mazingira hayo, basi hajui athari za kisheria endapo yaliyopo ndani ya mkataba yanapokiukwa. Mkataba wa Kim Poulsen na TFF ulikuwa unasema kocha huyo ndiye atakayeteua wachezaji wa Taifa Stars.
Pia mkataba huo ulikuwa unasema kocha huyo ni mwajiriwa wa TFF. Kwa vile Kim Poulsen alikuwa mwajiriwa wa TFF, na TFF kutaja timu haikuwa na athari kwa Kim kama ambavyo timu ingetangazwa na kocha mwingine wakati yeye bado yupo ndani ya mkataba.
Utawala bora ni pamoja na kuheshimu mkataba uliopo kati ya pande husika. Bila kusahau kuwa hakuna mkataba usiotoa mwanya (option) wa kuvunjwa.
Hivyo, Taifa Stars itaendelea kuwa ya kocha kwani ndiye anayeteua wachezaji kulingana na mtazamo wake na aina ya mfumo anaotumia. Siku zote kocha huchagua wachezaji wanaoendana na mfumo wake wa uchezaji.
Timu ikifanya vibaya ndiye anayebeba lawama, kama ambavyo anapongezwa pale inapofanya vizuri. Taifa Stars itaendelea kuwa ya Watanzania huku TFF tukiendelea kuwa wasimamizi wa timu hiyo.
Mwandishi ni Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na anapatikana kwa email: [email protected]