Prime
Ulimwengu ni suala la muda Singida
Muktasari:
- Hilo ni wazi kwani wapo mbioni kukamilisha usajili wa mshambuliaji Thomas Ulimwengu ambaye alikuwa anacheza kikosi cha TP Mazembe.
MABOSI wa klabu ya Singida Fountain Gate hawatanii kwani wanaonyesha wazi wanataka kutoshiriki tu kwenye mashindano ya kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao bali ni kwenda kushindana.
Hilo ni wazi kwani wapo mbioni kukamilisha usajili wa mshambuliaji Thomas Ulimwengu ambaye alikuwa anacheza kikosi cha TP Mazembe.
Ulimwengu kwa sasa ni mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na Mazembe.
Habari ambazo gazeti hili linazo ni kwamba mchezaji huyo na mastaa wengine ambao hawajatambulishwa tayari wapo kwenye mazoezi ya timu hiyo yanayoendelea mkoani Arusha kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya.
Chanzo kutoka ndani ya Singida kililidokeza gazeti hili kwamba Ulimwengu ni sehemu ya wachezaji ambao wanafanya mazoezi na kikosi hicho jijini Arusha.
"Kweli yupo huku na yeye ni miongoni mwa wachezaji wapya ambao bado hawajatambulishwa," kilisema chanzo hicho.
Bado haijawa wazi mchezaji huyo mwenye uwezo wa kucheza winga zote na mshambuliaji wa kati kama tayari amesaini mkataba au laa lakini ni wazi hawezi kuripoti kambini huku akiwa bado hajasaini mkataba wowote na timu hiyo.
Ulimwengu katika kikosi hicho ni wazi anaweza asisaini muda mrefu kwani ni kama vile mtu anayehitaji kupata muda wa kucheza kisha kuendelea na maisha yake ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi kwani alikuwa nje ya uwanja kwa miezi sita.
Kama Ulimwengu atasaini mkataba wa kuitumikia timu hiyo basi ni wazi itakuwa mara ya kwanza kwa mchezaji huyo kucheza soka la kulipwa nchini.
Upande wa Singida ni wazi usajili wa Ulimwengu unaenda kuongeza kitu katika kikosi chao kwani mchezaji huyo akiwa fiti anakuwa na ubora mzuri wa kuweka mipira wavuni.
Kingine ambacho kinambeba ni uzoefu wake wa mashindano makubwa kwani alishachukua ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2014/15 na alicheza Fainali za kombe la Dunia upande wa klabu 2016 akiwa na TP Mazembe.
Ulimwengu nje ya TP Mazembe alicheza katika timu za AFC Eskilstuna (Sweden), Sloboda Tuzla (Bosnia), Al Hilal (Sudan) na JS Saoura.