Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ULIMWENGU-3 : Kwaheri Congo, Ulaya hodii

Thomas Ulimwengu

Muktasari:

Kufikia katika hatua hii ya mazungumzo, huku tukiendelea kutazama filamu ya kusisimua kwa pamoja, Ulimwengu anapata sura ya huzuni na tabasamu linatoweka katika uso wake. Kwa nini? Kwa jinsi ambavyo tajiri wa TP Mazembe alibania ofa zake nyingi.

“Sina mpango wa kusaini mkataba mpya TP Mazembe. Sina kabisa mpango huo. Mkataba wangu unamaliza Julai na nina ofa kutoka katika klabu mbalimbali Ulaya kama vile Norway, Ubelgiji, Ufaransa na kwingineko na ni timu za Ligi Kuu,” anasema Ulimwengu.

Kufikia katika hatua hii ya mazungumzo, huku tukiendelea kutazama filamu ya kusisimua kwa pamoja, Ulimwengu anapata sura ya huzuni na tabasamu linatoweka katika uso wake. Kwa nini? Kwa jinsi ambavyo tajiri wa TP Mazembe alibania ofa zake nyingi.

“Ni wakati wa kwenda Ulaya sasa. Moise kabania sana ofa zetu. Unakuta kuna klabu inatuma ofa kwake lakini hawezi kukwambia. Ukichunguza unaambiwa ofa ilifika ofisini kwake na wala hakuambii na wala hana mpango wa kukuuza,” anakiri Ulimwengu.

“Kuna wakati unaomba akutoe hata kwa mkopo lakini anagoma. Sasa hivi klabu nyingi zinaishia kumjaribu tu lakini zinajua kwamba hawezi kutuuza. Hata hivyo, klabu hizo zinajua kwamba mikataba yetu (yeye na Mbwana) inaisha kwa hiyo hakuna shida,” anaongeza Ulimwengu.

Licha ya kukaribia kwenda Ulaya, Ulimwengu anadai kwamba kwa sasa hana wakala ila ana meneja wake, Roland ambaye amekuwa akiwasiliana naye mara kwa mara akimshauri katika mambo mengi na pia kumpa mwongozo.

“Sina wakala. Mawakala wengi sana ni matapeli. Mimi nina meneja tu, Roland. Unajua watu wengi hawaelewi tofuti kati ya wakala na meneja. Kwa sasa mimi nina meneja tu. Mawakala siwataki kwa sababu wanawakwamisha wachezaji wengi sana. Utakuta wakala anamsainisha mchezaji mkataba lakini wala hamtafutii timu mchezaji. Ukipata timu ndio anajitokeza. Sasa huyo amekusaidia nini?” anahoji Ulimwengu.

“Tunachofanya kwa sasa ni kuingia mkataba maalumu na wakala akutafutie timu, akishindwa basi lakini si mkataba wa kujifunga kwake halafu anashindwa kukutafutia timu kwa muda mrefu si sawa na ndiyo maana sina wakala. Timu zinajua namna ya kutupata kupitia mawakala wao wenyewe.”

TP Mazembe ni miongoni mwa klabu zinazolipa mishahara mikubwa kwa wachezaji wake barani Afrika. Wakati mwingine inahitaji moyo kuihama klabu hii inayoendeshwa na mtu ambaye ni tajiri wa migodi ya dhahabu na biashara lukuki huku akiwa ni Gavana wa Jimbo la Katanga, Moise Katumbi.

Kuna madai kuwa kuna wachezaji wengi wa Mazembe kama kina Robert Kidiaba, Jean Kasusura, Reinford Kalaba na wengineo wamefikia viwango vya kucheza soka katika ligi mbalimbali za Ulaya lakini wanabaki Mazembe kwa sababu ya pesa.

“Pesa siyo tatizo sana,” anakiri Ulimwengu “Nataka kwenda Ulaya kwa sababu ni kitu ambacho nimejiwekea kwa muda mrefu. Ni kweli pesa tunapata sana lakini malengo ni kucheza Ulaya. Hata hivyo, mbona kuna timu za Ulaya zinatutaka zinalipa sana kuliko Mazembe?” anahoji Ulimwengu ambaye anatambulika kirahisi uwanjani kwa sababu ya staili yake ya nywele ya kiduku.

“Hawa kina Kidiaba siwezi kuwasemea lakini naona wao wameridhika tu kucheza Mazembe na inawezekana labda kwa sababu umri wao umesogea kidogo. Stopilla (Sunzu) alikwenda Ulaya kwa sababu nadhani aliangalia mbali zaidi kucheza huko.”

Akiwa tayari ameshacheza Ulaya na pia akiwa na uzoefu na soka la Afrika katika klabu iliyo anga za juu kama TP Mazembe, Ulimwengu anakiri kuwa bado mazingira ya kucheza soka la kulipwa Ulaya ni mazuri zaidi kuliko Mazembe.

“Ulaya ni Ulaya tu asikwambie mtu. Mazingira kama ya ile klabu ya Sweden niliyokuwa nafanyia mazoezi ni mazuri sana. Ukijituma unaona kabisa kuwa unaweza kufika mbali na ukifika mbali malipo yake ni makubwa kuliko Mazembe.”

Ulimwengu anakiri kwamba hata akipokea ofa za timu kubwa za Afrika kama Etoile du Sahel, Esperance, Al Alhy na nyinginezo hataki kuhamia timu hizo kwa sababu hana mpango tena wa kuendelea kusakata soka barani Afrika.

“Ni afadhali hata nibakie Congo kuliko kwenda kucheza katika timu hizo. Kwa sasa akili yangu yote ipo katika kucheza soka la kulipwa Ulaya na si Afrika tena,” anaendelea Ulimwengu.

Ndoto za kucheza Ulaya zinaweza kuwa mwisho wa uswahiba wa karibu kwa Ulimwengu na Mbwana. Wamekuwa kama ndugu ndani na nje ya uwanja na mara zote wamekuwa wakiandamana popote wanapokwenda. Urafiki wao ulianzia katika timu ya taifa ya vijana kwa sababu Mbwana hakucheza katika timu ya kituo cha watoto cha TFF, TSA.

“Mimi nina ofa tofauti na za Mbwana. Yeye kuna timu nyingine zinazomsaka na mimi nina timu nyingine ambazo zinanisaka. Hakuna timu ambayo imeonyesha nia ya kutuchukua wote wawili kwa pamoja,” anaongeza Ulimwengu.

Wakati Ulimwengu na Mbwana wakisifika kwa kuibeba timu ya taifa ya Tanzania kwa kile kinachoonekana kuwa mbinu za kisasa zaidi, namuuliza Ulimwengu ni wachezaji gani wa Tanzania ambao anaamini kuwa wanaweza kuungana na wao kwa kucheza soka la kulipwa nje ya mipaka yao kwa sasa.

Je ni wachezaji gani ambao Ulimwengu amewataja? Ni kweli anaamini kuwa kuna wachezaji wa Kitanzania wanaoweza kutamba nje ya mipaka yao kama inavyotokea kwake na kwa Mbwana Samatta kwa sasa? Usikose mahojiano ya staa huyu na Mwandishi wa Mwanaspoti, Edo Kumwembe yaliyofanyika Blantyre Malawi wiki iliyopita siku ya Jumatatu.