Ukweli kuhusu Wydad kuikomalia Simba dili la Mwalimu
Muktasari:
- Wakati Simba ikitangaza usajili huo, viongozi wa Wydad walipofanya uhakiki wa miamala kwenye akaunti yao rasmi hawakuona fedha zozote zikiwa zimeingia. Hata hivyo uchunguzi ulibaini malipo hayo yalikuwa yamepelekwa kwenye akaunti ya zamani ya klabu hiyo ambayo tayari ilikuwa imebadilishwa.
SIMBA haikukurupuka kumtambulisha Selemani Mwalimu. Kilichotokea ni kwamba mabingwa hao wa Kombe la Shirikisho la CRDB waliamini kila kitu kilikuwa kimekamilika baada ya kutuma fedha za mkataba wa mkopo, lakini baadaye ikabainika malipo hayo yaliingia kwenye akaunti ya zamani ya Wydad AC, jambo lililosababisha miamba hiyo ya Morocco kutangaza mshambuliaji huyo bado ni sehemu ya kikosi chao kwa msimu ujao.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata kutoka kwa mtu wa karibu na mchezaji huyo, zinaeleza Simba na Wydad tayari walikuwa wamefikia makubaliano ya Mwalimu kuendelea kubaki Msimbazi kwa mkopo wa mwaka mmoja, huku upande wa Simba ukitekeleza masharti ya awali kwa kutuma fedha zilizokubaliwa.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, baada ya kukamilisha hatua hiyo, Simba iliamini dili hilo limekamilika na ndipo ikamtangaza hadharani Mwalimu kama sehemu ya kikosi chake kitakachoshiriki msimu ujao wa mashindano.
Wakati Simba ikitangaza usajili huo, viongozi wa Wydad walipofanya uhakiki wa miamala kwenye akaunti yao rasmi hawakuona fedha zozote zikiwa zimeingia. Hata hivyo uchunguzi ulibaini malipo hayo yalikuwa yamepelekwa kwenye akaunti ya zamani ya klabu hiyo ambayo tayari ilikuwa imebadilishwa.
"Makubaliano yalishafanyika na Simba walikuwa wametekeleza upande wao. Tatizo lilikuwa fedha kuingia kwenye akaunti ya zamani ya Wydad walipoangalia akaunti wanayotumia sasa hawakuona malipo yoyote, ndipo wakaamini dili halijakamilika na kutoa taarifa kwamba mchezaji bado ni sehemu ya kikosi chao," kilisema chanzo hicho.
Hayo yote yanajiri baada ya leo Julai 22, 2026 Wydad kutoa taarifa kuhusu kutotambua makubaliano hayo na kuzua taharuki kwenye mitandao ya kijamii huku baadhi ya mashabiki wakijiuliza ni ipi taarifa sahihi kati ya ile ya Simba iliyomtambulisha Mwalimu na ile ya mabingwa hao wa Morocco waliodai bado wanamuhitaji mshambuliaji huyo.
Taarifa zinaeleza kuwa pande zote mbili zinafanyia kazi kurekebisha hitilafu hiyo ya kifedha kwa kuzirejesha fedha kutoka kwenye akaunti ya zamani ili ziingizwe kwenye akaunti mpya ya Wydad.
Mchakato huo ukikamilika, klabu hiyo ya Morocco inatarajiwa kuthibitisha rasmi makubaliano ya kumruhusu Mwalimu kuendelea kuitumikia Simba kwa mkopo wa mwaka mmoja.
Chanzo hicho kinasisitiza kuwa hakuna mgogoro wowote kati ya Simba na Wydad kuhusu mchezaji huyo, bali kilichotokea ni hitilafu ya kiutawala katika miamala ya fedha.
Simba iliamua kupambana kumbakiza Mwalimu baada ya kuridhishwa na kiwango alichoonyesha msimu uliopita. Mshambuliaji huyo alikuwa mmoja wa nyota muhimu wa kikosi hicho baada ya kufunga mabao 15 katika mashindano yote, akitoa mchango mkubwa kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara na mashindano ya kimataifa.