Uhamiaji haishikiki Ligi Kuu Zanzibar
Muktasari:
- Katika msimu huu wa 2026-2027, timu hiyo imefanikiwa kucheza mechi nne huku ikishinda zote, ikiongoza pia kwa kufunga mabao mengi ambayo ni tisa.
TIMU ya Uhamiaji inayoshiriki Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), imeendelea kushikilia rekodi yake ya kuongoza msimamo wa ligi hiyo katika mechi nne za awali.
Katika msimu huu wa 2026-2027, timu hiyo imefanikiwa kucheza mechi nne huku ikishinda zote, ikiongoza pia kwa kufunga mabao mengi ambayo ni tisa.
Uhamiaji yenye maskani yake kisiwani Unguja, mechi yake ya kwanza iliifunga Wembe bao 1-0, kisha ikaisulubu Chipukizi mabao 4-1, ikaenda Pemba na kuipiga Fufuni mabao 2-0 na kumalizia kwa kuitandika Mwenge 2-0 hukohuko Pemba.
Hadi kufikia sasa, katika mechi nne ilizocheza Uhamiaji, nyavu za timu hiyo zimetikiswa mara moja pekee na Chipukizi, bao hilo likifungwa na kiungo Mshambuliaji Daddy Francis.
Kocha Mkuu wa Uhamiaji, Sheha Khamis, amesema licha ya kukusanya pointi hizo bado haikuwa rahisi upande wao kwani timu zote zilijipanga vya kutosha.
Amesema, bado anawasisitiza wachezaji wa timu hiyo kuendelea kupambana bila kuchoka kwani ligi ni ngumu, hivyo waungane kuanza na kumaliza msimu vizuri.
Wakati Uhamiaji ikiwa kileleni, kabla ya mechi ya jana nafasi ya pili ilikuwa ikishikiliwa na Kipanga yenye pointi nane sawa na Polisi iliyo nafasi ya tatu, huku Kipanga na JKU zikiwa na pointi saba katika nafasi ya nne na tano.