Uhamiaji bado inasukwa
Muktasari:
- Sheha alibainisha kwamba, ligi ya msimu huu ni ngumu, hivyo hahitaji kuanza vibaya na kupata shinda mbele ya safari ndio maana anafanya kila linalowezekana kuitengeneza timu kuwa bora wakati wote.
KOCHA MKUU wa Uhamiaji, Sheha Khamis amesema timu hiyo licha ya kupata ushindi katika mechi mbili ilizocheza katika Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) msimu huu, lakini itaendelea kujipanga vyema kuhakikisha inazidi kuimarika.
Sheha alibainisha kwamba, ligi ya msimu huu ni ngumu, hivyo hahitaji kuanza vibaya na kupata shinda mbele ya safari ndio maana anafanya kila linalowezekana kuitengeneza timu kuwa bora wakati wote.
Kabla ya mechi za jana Jumatano, Uhamiaji ilukuwa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikikusanya pointi sita sawa na Muembe Makumbi na Polisi, lakini tofauti ya mabao imewabeba.
“Kitu tunachokikosa kwenye mechi zetu ni wachezaji kutokuwa na utulivu jambo ambalo linatukosesha mabao mengi wakati tun apotengeneza nafasi,” alisema kocha huyo ambaye kikosi chake kimefunga mabao matano na kuruhusu moja.
Alisema, kipindi hiki ligi inapoendelea, pia anakisuka kikosi kwa kurekebisha makosa waliyofanya kwenye mechi mbili zilizopita kuhakikisha wanapotengeneza nafasi zinazaa matunda.
Kocha huyo alisema anatumia uzoefu wake kuijenga timu hiyo kuwa na ushindani kwa kuleta ladha tofauti kwenye Ligi Kuu ya Zanzibar, huku akiahidi kutowaangusha viongozi waliompa imani ya kukiongoza kikosi cha Uhamiaji.
Uhamiaji baada ya kucheza mechi mbili nyumbani huko Unguja na kushinda zote dhidi ya Wembe (1-0) na Chipukizi (4-1), sasa imeelekea Pemba kukabiliana na Mwenge (Septemba 13, 2026) na Fufuni (Septemba 16, 2026), mechi zote zikipangwa kuchezwa Uwanja wa Gombani.