Uchaguzi mkuu Simba Januari 3, 2027
SIMBA imetangaza ratiba ya uchaguzi mkuu wa klabu hiyo, ambapo zoezi la kupiga kura linatarajiwa kufanyika Januari 3, 2027, baada ya kukamilika kwa hatua mbalimbali za mchakato huo, zikiwemo uchukuaji na urejeshaji wa fomu, uhakiki wa wagombea, usikilizwaji wa mapingamizi na kampeni.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Simba, Anderson Msumba, amesema uchaguzi huo unafanyika kwa kuzingatia katiba ya klabu na kanuni za uchaguzi.
“Kwa mujibu wa Katiba ya Simba ya mwaka 2018, ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2025 na kusajiliwa Februari 2026, uchaguzi unatakiwa kufanyika kila baada ya miaka minne, kwa mujibu wa Ibara ya 26. Uchaguzi wa mwisho wa Simba ulifanyika Januari 2023, hivyo ukomo wa uongozi wa sasa ni Januari 2027,” amesema Msumba.
Ameongeza kuwa, kamati imeweka wazi utaratibu mzima wa uchaguzi, kuanzia tangazo, uchukuaji na urejeshaji wa fomu, uhakiki wa wagombea, kampeni hadi siku ya kupiga kura.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Simba, Alpha Honest Gervas, amesema uchukuaji wa fomu za kugombea nafasi mbalimbali utaanza Oktoba 30 hadi Novemba 6, 2026, huku urejeshaji wa fomu hizo ukifanyika Novemba 7 hadi 11 mwaka huu.
Gervas amesema uhakiki wa fomu utafanyika Novemba 12 hadi 14, 2026, kabla ya majina ya wagombea waliokidhi vigezo kutangazwa na kuanza kwa mchakato wa mapingamizi.
“Tarehe 30 Oktoba hadi Novemba 6, 2026, litakuwa zoezi la kuchukua fomu kwa wagombea, huku Novemba 7 hadi 11 ikiwa ni kipindi cha kurejesha fomu. Novemba 12 hadi 14 tutapitia, kukagua na kuhakiki fomu ili kubaini kama zimejazwa kwa usahihi na wagombea wamekidhi vigezo,” amesema Gervas.
Alifafanua kuwa Novemba 15, 2026 itakuwa siku ya kutangaza majina ya awali ya wagombea waliokidhi vigezo na kupokea mapingamizi dhidi yao.
“Tarehe 17 na 18 Novemba tutapokea mapingamizi, Novemba 19 hadi 21 tutayapitia na kuandaa hati za wito kwa wahusika. Usikilizwaji wa mapingamizi utafanyika Novemba 23 hadi 25, huku maamuzi yakitolewa Novemba 26 na 27. Majina ya mwisho ya wagombea waliofuzu yatatangazwa Novemba 30, 2026,” ameongeza.
Gervas amesema kampeni za wagombea zitaanza Desemba 3, 2026, hadi Januari 2, 2027, kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika Januari 3, 2027.
LAZIMA SHAHADA
Katika hatua nyingine, Mjumbe wa Kamati ya Uchaguzi ya Simba, Richard Daudi Mwalwiba amefafanua vigezo vya elimu na sifa nyingine zinazotakiwa kwa wanachama wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya klabu hiyo.
Mwalwiba amesema kwa mujibu wa ibara ya 27 ya Katiba ya Simba, mgombea wa nafasi ya mwenyekiti anatakiwa kuwa na shahada ya chuo kikuu.
“Kulingana na Ibara ya 27 ya Katiba ya Simba, nafasi za uongozi zimeainishwa, ambapo nafasi tano zitagombewa na nafasi mbili zitajazwa kupitia uteuzi wa mwenyekiti atakayechaguliwa. Kwa nafasi ya mwenyekiti, mgombea anatakiwa angalau awe na shahada ya chuo kikuu,” amesema Mwalwiba.
Alifafanua kuwa nafasi tano zinazogombewa zinahusisha uwakilishi wa wanachama wanaoishi nje ya Tanzania, huku nafasi moja kati ya hizo ikitengwa kwa mwanamke.