Simba, Yanga zapewa makundi ya visasi CAF
Muktasari:
- Katika makundi hayo, timu hizo zimekutanishwa na wapinzani wengi ambao wamewahi kupata matokeo mazuri dhidi ya wawakilishi hao wa Tanzania.
Simba na Yanga zimejikuta zikiangukia katika makundi yenye shauku ya visasi katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Katika droo ya mashindano hayo iliyofanyika leo Jumatano, Oktoba 28, 2026 jijini Cairo, Misri, Yanga imepangwa kundi B na Simba imepangwa kundi C.
Katika makundi hayo, timu hizo zimekutanishwa na wapinzani wengi ambao wamewahi kupata matokeo mazuri dhidi ya wawakilishi hao wa Tanzania.
Hivyo hii inaweza kuwa fursa nzuri kwa Yanga na Simba kulipa kisasi huku zikisaka ushindi wa kuziweka katika mazingira mazuri ya kutamba kwenye mashindano hayo.
Mara ya kwanza, Yanga ilikutana na Zamalek mwaka 2000 kwenye raundi ya kwanza ya Kombe la Washindi Afrika ambapo ilitolewa kwa kufungwa mabao 5-1.
Mara ya pili ilikuwa ni mwaka 2012 katika raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo Yanga ilitolewa kwa kufungwa mabao 2-1 na timu hiyo ya Misri.
Mara ya mwisho kwa Yanga kukutana na MC Alger ilikuwa ni katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2024/2025.
Katika mechi iliyochezwa hapa Dar es Salaam, timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana na ziliporudiana nchini Algeria, Yanga ilifungwa mabao 2-0.
Yanga na Club African zilikutana katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022/2023 kwenye raundi ya mchujo ambapo Yanga ilisonga mbele ikitoka sare ya bao 1-1 nyumbani na kushinda bao 1-0 ugenini.
Kwa upande wa Simba, itakutana na Orlando Pirates na RS Berkane ambazo zimewahi kumtoa katika awamu tofauti.
Mara ya mwisho kwa Simba kukutana na RS Berkane ilikuwa ni katika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2024/2025 ambapo Berkane ilitwaa ubingwa.
Zilipocheza Morocco, Simba ilifungwa mabao 2-0 na zilipokutana Zanzibar katika mechi ya marudiano, zilitoka sare ya bao 1-1.
Orlando Pirates na Simba mara ya mwisho zilikutana msimu wa 2021/2022 katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Simba katika mechi ya kwanza nyumbani ilishinda bao 1-0 na ugenini ikafungwa bao 1-0 kisha kwenye mikwaju ya penalti, Orlando Pirates ikashinda kwa mikwaju ya penalti 4-3.
Colombe Sport ni timu mpya kwenye hatua hiyo.