Ubingwa Yanga Princess, Simba Queens uko hapa

Muktasari:

HATIMA ya klabu ya wanawake ya Simba Queens iko mikononi mwa Baobab Queens katika mchezo wa mwisho la lala salama ya Ligi ya wanawake Tanzania Bara inayotarajiwa kufikia tamati Mei 16 (Jumapili).

HATIMA ya klabu ya wanawake ya Simba Queens iko mikononi mwa Baobab Queens katika mchezo wa mwisho la lala salama ya Ligi ya wanawake Tanzania Bara inayotarajiwa kufikia tamati Mei 16 (Jumapili).

Simba ambaye ni bingwa mtetezi anakamilisha michezo yake akiwakabili Baobab katika dimba la Jamhuri Dodoma huku Yanga Princess wao  wakiumana na Alliance ya Jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo wa jana Simba  Queens ilifanya kufuru katika dimba la Mo Simba Arena na kuwafunga Mlandiz Queens mabao 4-0 yaliyofungwa na Mawete Musolo mabao mawili, Opa Clement bao moja na Jackline Albert.

Baada ya matokeo hayo ya jana Simba Queens wameendelea kujiweka katika nafasi nzuri ya kulitwaa taji hilo kwa mara nyingine msimu huu.

Michezo ya mwisho yoyote kati ya Simba Queens na Yanga Princess wanauhakika wa kulitwaa taji hilo kutokana na msimamo ulivyokuwa.

Simba Queens anaongoza ligi akiwa na pointi akiwa na pointi 51 baada ya kujitupa dimbani mara 19 akishinda michezo 16 sare tatu hajapoteza hata mmoja, huku Yanga akiwa na pointi 50 akishinda michezo 16 sare mbili na kupoteza mchezo mmoja.

Nafasi ya tatu inashikiliwa na JKT Queens wenye pointi 45 wakishinda michezo 15 sare hawana na kupoteza michezo minne huku nafasi ya nne Ruvuma Queens akiwa na pointi 31 akishinda tisa, sare nne na kupoteza sita.

Katika michezo ya mwisho Simba anatakiwa kuhakikisha anashinda dhidi ya Baobab ili kulitetea taji hilo,Yanga Princess nao wakipambana kushinda huku wakimuombea njaa Simba ili apoteze mchezo huo.

Iko hivi mpaka sasa Yanga ananafasi ya kulitwaa taji hilo endapo Simba atapoteza na yeye akashinda dhidi ya Alliance na ikitokea Yanga akatoka sare na Simba akapoteza tayari Simba atakuwa ametetea taji hilo kutokana na idadi kubwa ya mabao ya kufungwa na kufunga.