Straika Dodoma Jiji aendeleza rekodi
Muktasari:
- Katika misimu hiyo mitatu ambayo Edgar ameifunga TRA United, amecheza timu mbili tofauti ambapo alianza na Fountain Gate msimu wa 2024-2025, kisha misimu ya 2025-2026 na 2026-2027, akiichezea Dodoma Jiji. Kila mshambuliaji huyo anapofunga bao dhidi ya TRA United, upande wake haujawahi kupoteza mechi.
MSHAMBULIAJI wa Dodoma Jiji, Edgar William, ameendeleza rekodi bora ya kuvutia ya kuifunga TRA United katika mechi za Ligi Kuu Bara, baada ya nyota huyo kutikisa nyavu tena Agosti 29, 2026, ikiwa ni msimu wa tatu mfululizo anafanya hivyo.
Katika misimu hiyo mitatu ambayo Edgar ameifunga TRA United, amecheza timu mbili tofauti ambapo alianza na Fountain Gate msimu wa 2024-2025, kisha misimu ya 2025-2026 na 2026-2027, akiichezea Dodoma Jiji. Kila mshambuliaji huyo anapofunga bao dhidi ya TRA United, upande wake haujawahi kupoteza mechi.
Nyota huyo alianza kuonyesha makali yake msimu wa 2024-2025, wakati Fountain Gate ilipoichapa Tabora United kwa sasa TRA United mabao 3-1, katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora, Septemba 20, 2024.
Katika mechi hiyo, Edgar alifunga mabao mawili dakika ya 37 na 90 na lingine moja la Fountain Gate likifungwa na Salum Kihimbwa kwa penalti dakika ya 26, huku bao la kufutia machozi la TRA United, lilifungwa na Yacouba Songne dakika ya 77.
Msimu wa 2025-2026, mshambuliaji huyo akahamia Dodoma Jiji na kuendeleza rekodi hiyo baada ya kufunga bao moja katika ushindi wa 3-0 dhidi ya TRA United, Februari 12, 2026. Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, mabao ya Dodoma Jiji yalifungwa na Faraji Kayanda dakika ya 15, Gadiel Michael dakika ya 40 na Edgar William dakika ya 55 na kumaliza msimu huo akiwa na mabao saba.
Msimu huu mshambuliaji huyo ameendeleza makali yake baada ya kuifungia Dodoma Jiji bao pekee katika ushindi wa 1-0 dhidi ya TRA United, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh, Amri Abeid, Arusha.
Akizungumzia hilo, Edgar amesema ni jambo nzuri kuona mwendelezo wa rekodi hiyo ya kuvutia kwa manufaa ya timu kiujumla, ingawa kinachotokea ni bahati na sio kitu unachofikiria kinaweza kutokea mara nyingi, hasa kutokana na ushindani uliopo.