TPLB yatoa adhabu, waamuzi wafutwa Championship
Muktasari:
- Katika taarifa iliyotolewa leo, Oktoba 8, 2026, na Idara ya Habari na Mawasiliano ya TPLB, jumla ya makosa mbalimbali yameainishwa, huku baadhi ya klabu zikitozwa faini za fedha na wengine kupewa onyo kali.
BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeendelea kukaza kamba katika kusimamia nidhamu na uendeshaji wa Ligi ya Championship ya NBC msimu wa 2026/27, baada ya kutoa adhabu mbalimbali kwa klabu, viongozi, watendaji na waamuzi kutokana na makosa yaliyojitokeza katika michezo ya hivi karibuni.
Katika taarifa iliyotolewa leo, Oktoba 8, 2026, na Idara ya Habari na Mawasiliano ya TPLB, jumla ya makosa mbalimbali yameainishwa, huku baadhi ya klabu zikitozwa faini za fedha na wengine kupewa onyo kali.
Miongoni mwa klabu zilizoguswa ni Mbeya Kwanza, ambayo imetozwa faini ya Sh5 milioni baada ya kuchelewa kufika uwanjani katika mchezo dhidi ya Tanzania Prisons.
Klabu hiyo ilitakiwa kufika saa 8:30 mchana, lakini iliwasili saa 8:47, jambo lililoifanya ikumbane na adhabu hiyo.
Songea United nayo haikupita salama, ikitozwa faini ya Sh5 milioni kwa kuchelewa kufika uwanjani katika mchezo dhidi ya Rhino Rangers. Klabu hiyo ilifika saa 8:58 mchana badala ya muda uliopangwa.
Songea United pia imepewa onyo kali kutokana na kuchelewa kufika kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo (MCM) kabla ya kukutana na Tanzania Prisons.
MASHABIKI NAO WAGUSWA
Mbali na makosa ya klabu, TPLB imechukua hatua dhidi ya vitendo vya mashabiki vilivyoonekana kuvuka mipaka.
Mtibwa Sugar imepigwa faini ya Sh1 milioni baada ya mashabiki wake kumrushia mawe mwamuzi msaidizi namba mbili, Hudson Samwel, katika mchezo dhidi ya Mbeya Kwanza.
Bandari Tanzania yenyewe imekutwa na kosa la mashabiki wake kuingia ndani ya eneo la kuchezea baada ya mchezo dhidi ya KMC FC kumalizika, jambo lililoifanya itozwe faini ya Sh5 milioni.
‘VIMIMINIKA’ VYAWAGUSA
Katika hatua nyingine, TPLB imechukua hatua dhidi ya vitendo vilivyotafsiriwa kuwa vinahusiana na imani za kishirikina ndani ya uwanja.
Christopher Joseph, mtunza vifaa wa Mbuni, amepigwa faini Sh1 milioni baada ya kukutwa akimwaga vimiminika katika maeneo mbalimbali ya uwanja wakati timu zikiwa kwenye maandalizi ya mchezo.
Michael Mpesa wa Tanzania Prisons na Ezekiel Eusebio wa Mbuni nao wametozwa Sh1 milioni kila mmoja kwa kukataa kutoka uwanjani wakati wa mapumziko.
Kwa upande wa Songea United, viongozi Ramadhani Kapera na Gilbert Boniface pamoja na daktari wa timu, Shabani Mbotohii, kila mmoja ametozwa Sh1 milioni baada ya kukutwa wakimwaga vimiminika katika maeneo mbalimbali ya uwanja kabla ya mchezo dhidi ya Tanzania Prisons.
BALL BOYS WAWAINGIZA KIBARUA
Transit Camp nayo imeingia kwenye orodha ya waliokumbana na adhabu baada ya vijana wake wa kuokota mipira, maarufu ‘Ball Boys’, kutuhumiwa kuchelewesha kwa makusudi kurudisha mipira uwanjani wakati ilipotoka nje katika mchezo dhidi ya IAA SC.Kwa kosa hilo, klabu hiyo imepigwa faini ya Sh5 milioni.
Mbeya pia imepewa onyo kali kwa kushindwa kuandaa mchezo kikamilifu baada ya gari la wagonjwa kuchelewa kufika uwanjani kwa dakika 15 katika mchezo dhidi ya Bandari Tanzania.
WAAMUZI WAWILI WAFUTWA
Lakini pengine hatua kubwa zaidi ni kwa upande wa waamuzi, ambapo TPLB imeamua kuwaondoa kabisa kwenye orodha ya waamuzi wa Ligi ya Championship msimu huu.
Mwamuzi wa kati, Ikram Nguyahambi kutoka Tabora, pamoja na mwamuzi msaidizi namba moja, Haruna Shammea wa Tanga, wamefutwa kwenye orodha hiyo baada ya kubainika kuwa walionyesha mapungufu makubwa ya kiuchezaji na kushindwa kutafsiri ipasavyo sheria za mchezo.
Hatua hizi zinaonyesha msisitizo wa TPLB katika kuhakikisha ushindani wa Championship unaendeshwa kwa kuzingatia nidhamu, taratibu na sheria za mchezo ndani na nje ya uwanja bila kuvunja sheria yoyote.