Bao la Clara lachaguliwa kuwa bao bora la wiki
Muktasari:
- Clara aliingia kwenye kinyang’anyiro hicho baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika mechi ya timu hiyo dhidhi ya Houston Dash iliopigwa Oktoba 5, 2026.
MSHAMBULIAJI wa Tanzania, Clara Luvanga ameendelea kuandika historia kwenye soka la Marekani baada ya bao lake alilofunga wiki iliyopita kutyangazwa kuwa bao bora la wiki katika Ligi ya Wanawake Marekani akiwa na kikosi cha Washington Spirit.
Clara aliingia kwenye kinyang’anyiro hicho baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika mechi ya timu hiyo dhidhi ya Houston Dash iliopigwa Oktoba 5, 2026.
Katika mechi hiyo, Washington Spirit ilishinda mabao 3-2, lakini Clara alifunga bao moja la ushindi dakika ya 84 baada ya kuingia kipindi cha pili akicheza dakika 25.
Bao hilo ndilo lililomuingiza kwenye orodha ya wachezaji waliokuwa wakigombea tuzo ya bao bora la wiki alilokuwa anawania na nyota wengine wa NWSL walikuwa na ushindani mkubwa kupitia mabao yao katika mechi zilizopita.
Clara aliwashinda Miljana Ivanovic wa Houston Dash, Lia Godfrey wa San Diego Wave FC na Brecken Mozingo wa Utah Royals FC, huku mashabiki na wafuasi wa ligi hiyo wakipata nafasi ya kuchagua bao lililostahili kutwaa heshima hiyo kwenye mitandao ya kijamii.
Mchezo huo ulikuwa wa pili kwa Luvanga tangu asajiliwe na Washington Spirit Septemba 9, 2026, akitokea Al Nassr ya Saudi Arabia kwa mkataba wa miaka minne.
Katika mchezo wake wa kwanza, aliingia akitokea benchi dhidi ya Angel City FC Septemba 26, 2026 ambapo Washington Spirit ilifungwa bao 1-0 akicheza kwa dakika 24.
Huo ni mwanzo mzuri kwa Clara ambaye amesajiliwa na klabu hiyo huku uhamisho wake ukitajwa kugharimu kiasi kikubwa na kuvunja rekodi duniani.
Hizo ni dalili njema kwa Mtanzania huyo ambaye amekuwa na muendelezo mzuri tangu akiwa na kikosi cha Al Nassr ya Saudia msimu uliopita ambako aliibuka mfungaji bora wa ligi hiyo akiweka kambani mabao 24.
Akizungumza na Mwanaspoti Clara amesema “Kwangu ni kitu kizuri kuanza msimu na bao kwenye ligi ngumu kama Marekani ambayo ina wachezaji wengi wazuri,” amesema mchezaji huyo ambaye ameweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza mwanamke kucheza ligi hiyo.