Timu 20 vita ya kupanda daraja
Muktasari:
- Mashindano hayo yanatarajiwa kuanza Septemba 6, 2026, huku fainali ya safari hiyo ya kusaka tiketi za Ligi Kuu ikitarajiwa kufikia tamati Septemba 13, kwenye Uwanja wa Chuo cha Ualimu Tabora (TTC).
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limetangaza ratiba ya Ligi Daraja la Kwanza Wanawake (WFDL), huku timu 20 zikiingia kwenye vita ya kuwania nafasi mbili za kupanda Ligi Kuu Wanawake msimu wa 2026/27.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuanza Septemba 6, 2026, huku fainali ya safari hiyo ya kusaka tiketi za Ligi Kuu ikitarajiwa kufikia tamati Septemba 13, kwenye Uwanja wa Chuo cha Ualimu Tabora (TTC).
Timu hizo 20 zimegawanywa katika makundi mawili, huku kila moja ikipambana kuhakikisha inamaliza katika nafasi itakayoiwezesha kupanda daraja na kuungana na vigogo wa Ligi Kuu Wanawake msimu ujao.
Timu zitakazoshiriki ni Mbagala Queens na Rangi 3 Queens za Dar es Salaam, Ludewa SC ya Dodoma, Kanyonzwa Queens ya Kigoma, Kitulo Queens ya Njombe, Barikiwa Queens ya Simiyu, Tanga Women ya Tanga, Youngstars Academy ya Iringa, Victoria Women ya Kagera na Kahama SC ya Shinyanga.
Nyingine ni Bukongo Queens ya Mwanza, Manyoni SC ya Singida, Icon FC ya Mbeya, Kilimanjaro Plantation ya Kilimanjaro, Bagamoyo Sisters ya Pwani, Mteteu Sekondari ya Morogoro, IAA Princess ya Arusha, Kilwa Princess ya Lindi na Jasper Youth ya Geita.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na TFF, timu zote zinatakiwa kuwasili Tabora Septemba 5, siku ambayo pia itatumika kwa ajili ya uhakiki wa usajili wa wachezaji.
Siku inayofuata, Septemba 6, kutakuwa na kikao cha viongozi wa timu, waamuzi na madaktari, pamoja na kupitia ratiba ya mashindano, kabla ya mechi kuanza rasmi Septemba 7.
Michezo itaendelea hadi Septemba 13, huku Septemba 14 ikiwa imetengwa kwa ajili ya timu kuondoka Tabora na kurejea katika vituo vyao.
TFF YAGARAMIA MALAZI, CHAKULA
Katika kuhakikisha timu zinapata mazingira mazuri ya kushiriki mashindano hayo, TFF imesema itatoa huduma ya malazi na chakula kwa watu 25 kutoka kila timu.
Shirikisho hilo pia litagharamia nauli ya watu watano kutoka kila timu, kutoka kituo chao cha usafiri hadi Tabora na kurejea baada ya mashindano.
Wakati huo huo, TFF imewakumbusha waamuzi kuhakikisha wanachezesha mechi zilizowekwa rasmi kwenye mfumo wa FIFA Connect. Hatua hiyo inalenga kuzuia matumizi ya waamuzi ambao hawajakamilisha usajili wao katika mfumo huo.
Kwa TFF, msisitizo huo ni sehemu ya kuboresha usimamizi wa mashindano, kuhakikisha uteuzi wa waamuzi unafuata taratibu na kuimarisha uwazi.