Tanzania yafuzu nusu fainali
Muktasari:
- Tanzania ilianza mchezo kwa kasi na kupata bao la kwanza dakika ya 30 kupitia Bashiri Salum Kibaila aliyeukwamisha mpira uliorejea baada ya kugonga mwamba wa chini.
TIMU ya Taifa ya Tanzania ya vijana chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes imeendelea kung’ara kwenye michuano ya CECAFA U-20 baada ya kuichapa Ethiopia mabao 4-0 katika mchezo wa Kundi A uliochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, leo Jumamosi usiku.
Tanzania ilianza mchezo kwa kasi na kupata bao la kwanza dakika ya 30 kupitia Bashiri Salum Kibaila aliyeukwamisha mpira uliorejea baada ya kugonga mwamba wa chini.
Kibaila ameongeza bao la pili dakika za mwisho za kipindi cha kwanza baada ya kumalizia pasi ya Juma Sagwe.
Mshambuliaji huyo aliyekuwa na kiwango bora alitolewa mwanzoni mwa kipindi cha pili na nafasi yake kuchukuliwa na Farid Mzalendo, lakini hilo halikupunguza makali ya wenyeji ambao waliendelea kuishambulia Ethiopia.
Dakika ya 54, Juma Sagwe alifunga bao la tatu kwa Tanzania, kabla ya kuongeza jingine dakika tatu baadaye na kukamilisha ushindi wa mabao 4-0.
Ethiopia ilijaribu kurudi mchezoni katika kipindi cha kwanza, lakini nafasi kadhaa hazikuzaa matunda, huku mpira wa faulo uliopigwa na Kasaw Dawit Yirdaw ukigonga mwamba na kuikosesha timu hiyo bao.
Ushindi huo umeifanya Tanzania kufikisha pointi sita na kumaliza kileleni mwa Kundi A, baada ya awali kuifunga Rwanda mabao 3-0 katika mchezo wake wa kwanza.
Sasa Ngorongoro Heroes imetinga nusu fainali, ambapo itakutana na Burundi. Uganda, iliyoshinda Sudan 1-0, itakutana na Sudan katika nusu fainali nyingine.
Timu mbili zitakazofika fainali ndizo zitakazopata tiketi ya kushiriki Fainali za AFCON U-20, hivyo Tanzania sasa inahitaji ushindi mmoja zaidi kufungua mlango wa kufuzu mashindano hayo.