Tanzania kuanza na Rwanda CECAFA U-20
Muktasari:
- Tanzania iko Kundi A pamoja na Rwanda na Ethiopia, katika mashindano ambayo timu tisa zinawania nafasi mbili za kuiwakilisha CECAFA kwenye fainali za U-20 AFCON zitakazofanyika mwakani nchini Ghana.
TIMU ya Taifa ya vijana U-20, Ngorongoro Heroes leo inaanza safari ya kutetea taji la mashindano ya Afrika Mashariki na Kati CECAFA U-20 dhidi ya Rwanda mechi itakayopigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Tanzania iko Kundi A pamoja na Rwanda na Ethiopia, katika mashindano ambayo timu tisa zinawania nafasi mbili za kuiwakilisha CECAFA kwenye fainali za U-20 AFCON zitakazofanyika mwakani nchini Ghana.
Mchezo wa Tanzania na Rwanda utapigwa saa 2:00 usiku mechi inayotarajiwa kuwa kivutio kikubwa, hasa kutokana na wenyeji kuhitaji kuanza kwa nguvu mbele ya mashabiki wao. Tanzania iliibuka bingwa wa michuano ya CECAFA U-20 iliyopita mwaka 2024, baada ya kuifunga Kenya 2-1 kwenye fainali, hivyo safari hii presha ipo juu ya Ngorongoro Heroes.
Kabla ya pambano hilo la Tanzania na Rwanda, zitapigwa mechi mbili Uganda dhidi ya Djibouti saa 8:00 mchana. Uganda, ikiwa Kundi B pamoja na Sudan na Djibouti, itaingia ikiwa na shinikizo la kuonyesha uwezo wake mapema, huku Djibouti ikitazama kupata matokeo yatakayoiweka kwenye nafasi ya kuvuka hatua zinazofuata.
Mechi nyingine itawakutanisha Sudan Kusini na Burundi saa 11:00 jioni, mchezo unaofungua kampeni ya Kundi C ambalo pia lina Kenya. Kwa kuwa timu zote zinahitaji kujiweka kwenye nafasi nzuri mapema, pambano hilo linaweza kutoa picha ya ushindani utakavyokuwa katika kundi hilo.
Akizungumza na Mwanaspoti nahodha wa Ngorongoro, Arafat Ally anayekipiga ENNPI inayoshiriki Ligi Kuu Misri amesema mashindano hayo ni jukwaa kubwa la kuonyesha uwezo na viwango vyao.
“Tunashukuru hadi sasa tukiwa salama, CECAFA ni mashindano makubwa kwa sababu yanazikutanisha timu za ukanda huu hivyo kwetu wachezaji tunayachukulia mashindano hayo kama jukwaa la kuonyesha vipaji vyetu,” amesema Arafat na kuongeza
“Tunajua tuna kibarua kikubwa mbele yetu dhidi ya Rwanda ambao ni miomngoni mwa timu ngumu na zenye ubora mkubwa hivyo kile ambacho ametuambia kocha wetu tutafuata kuhakikisha tunaondoka na pointi tatu.”