Ngorongoro Heroes iko tayari kwa AFCON
Muktasari:
- Nahodha wa Ngorongoro Heroes, Arafat Ally amesema lengo la kwanza la timu hiyo ni kubeba ubingwa utakaowapa tiketi ya kufuzu fainali hizo zitakazofanyika Ghana.
TIMU ya Taifa ya Tanzania ya vijana chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes, imedhamiria kufanya vizuri katika mashindano ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana, AFCON U-20 Kanda ya CECAFA.
Nahodha wa Ngorongoro Heroes, Arafat Ally amesema lengo la kwanza la timu hiyo ni kubeba ubingwa utakaowapa tiketi ya kufuzu fainali hizo zitakazofanyika Ghana.
Arafat amesema maandalizi yao yamekwenda vizuri na wachezaji wanaingia kwenye michuano hiyo wakiwa na morali kubwa ya kuwakilisha Tanzania. Amesema pamoja na kutambua ukubwa wa jukumu walilonalo, wamejipanga kufanya vizuri kuanzia mechi ya kwanza.
Arafat amesema Ngorongoro Heroes haijaingia kwenye mashindano hayo kushiriki tu, bali ina malengo makubwa ya kutwaa ubingwa wa Kanda ya CECAFA na kufuzu AFCON U-20.
Amesema mafanikio hayo yatawapa nafasi ya kwenda kushindana kwenye hatua kubwa zaidi ya Afrika na kuongeza uzoefu kwa vijana hao.
“Kwa maandalizi tumejiandaa vizuri, tunaahidi kufanya vizuri na tuna malengo kuchukua ubingwa halafu tufuzu kwenda AFCON, tuna majukumu makubwa ya kubeba taji la mashindano hayo,” amesema Arafat.
Kocha mkuu wa kikosi hicho, Mario Rivera Campesino amesema wako tayari kwa ajili ya kuanza kibarua hicho, huku akitambua ushindani utakuwa mkubwa kutokana na ubora wa timu zinazoshiriki.
Rivera amesema Rwanda ambayo Tanzania itakutana nayo katika mechi ya kwanza, ni miongoni mwa timu ngumu, hivyo wanahitaji kuwa makini.
Kocha huyo amesema kwa sasa akili zao zote zimeelekezwa kwenye mchezo dhidi ya Rwanda, wakiamini ushindi katika mchezo huo utawapa mwanzo mzuri wa safari yao kwa ajili ya malengo waliyojiwekea.
“Tupo tayari kwa ajili ya mashindano. Rwanda ni miongoni mwa timu ngumu na malengo yetu ni kushinda mechi yetu dhidi yao,” amesema Rivera.
Tanzania itakuwa mwenyeji wa michuano ya AFCON kwa vijana ukanda wa CECAFA, itakayofanyika kuanzia Septemba 15, 2026 hadi 24, 2026 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Michuano hiyo itazikutanisha timu tisa kutoka ukanda wa Afrika Mashariki, huku timu mbili zitakazofanya vizuri zaidi zikifuzu kuiwakilisha CECAFA katika fainali za AFCON U-20 zitakazofanyika Ghana 2027.
Tanzania, ambayo ni mabingwa watetezi wa U-20 katika ukanda wa CECAFA, imepangwa Kundi A pamoja na Ethiopia na Rwanda. Kundi B lina Uganda, Sudan na Djibouti, wakati Kundi C likiwa na Sudan Kusini, Kenya na Burundi.