Taifa Stars fainali tatu, pointi tatu
TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imeaga michuano ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023, ikiwa imeandika historia, huku kaimu kocha mkuu, Hemed Suleiman 'Morocco' akiweka bayana kitu kilichoiangusha timu hiyo kwenye fainali za msimu huu ambazo Stars ilionekana kama ingeenda 16 Bora.
Tuanzie na kilichowekwa historia na Stars katika michuano ya Afcon. Kama hujui hii ni mara ya tatu kwa timu hiyo kushiriki fainali hizo ikianza na zile za mwaka 1980 zilizofanyikia Nigeria, kisha 2019 pale Misri na safari hii ikaenda Ivory Coast, na rekodi zinaonyesha katika fainali hizo zote tatu Stars imevuna pointi tatu.
Katika fainali za mwaka 1980, Stars ikiwa Kundi A ilianza kwa kufungwa mabao 3-1 na Nigeria, kisha ikalala 2-1 kwa Misri na kutoka sare ya 1-1 na Ivory Coast, hivyo kupata pointi moja katika mechi tatu za kwanza, kisha ikakaa kwa miaka 39 kabla ya kurejea tena kwenye fainali za 2019 zilizofanyika Misri.
Kwenye fainali hizo Stars ilianza kwa kufungwa mabao 2-0 na Senegal, kisha kuchapwa mabao 3-2 na Harambee Stars ya Kenya kabla ya kuzabuliwa mabao 3-0 na walioibuka mabingwa, Algeria na timu hiyo kuaga michuano hiyo bila kupata ushindi wala pointi yoyote.
Katika fainali za safari hii zinazoingia hatua ya 16 Bora, Stars ilianza kwa kufungwa 3-0 na Morocco, kisha ikatoka sare ya 1-1 na Zambia kabla ya kusuluhu na DR Congo na kuifanya iage ikiwa na pointi mbili na hivyo kuifanya Tanzania katika fainali tatu ilizocheza iwe imevuna pointi tatu.
Sio pointi tatu tu, lakini Stars imecheza fainali hizo tatu ikifunga mabao sita kupitia wachezaji wanane, na yenyewe kuruhusu kufungwa mabao 18.
Wachezaji walioandika majina yao kwenye fainali hizo tatu ni Juma Mkambi ambaye kwa sasa ni marehemu aliyefunga kwenye mechi ya kwanza ya Tanzania kucheza Afcon 1980 ilipocharazwa 3-1 na wenyeji Nigeria, kisha Thuwen Ally Wazir kufunga mabao mawili kwenye mechi zilizofuata ambapo Tanzania ililala 2-1 kwa Misri na kutoka sare ya 1-1 na Ivory Coast.
Katika fainali za mwaka 2019, Simon Msuva na Mbwana Samatta ndio waliofunga mabao pekee iliyotoka nayo timu hiyo Misri, huku kwa msimu huu bao pekee la Tanzania lilifungwa na Msuva tena akiwa ni mchezaji aliyefunga kwenye fainali mbili mfululizo za Stars, akilingana sasa na Thuwen Ally Wazir.
MSIKIE MOROCCO
Kaimu Kocha Mkuu wa Stars, Hemed Suleiman 'Morocco' aliyekuwa na timu hiyo katika fainali mbili mfululizo za 2019 akiwa chini ya Emmanuel Amunike na sasa Adel Amrouche, alifichua kilichoiangusha timu hiyo kwenye fainali za mwaka huu zilizofanyika Ivory Coast.
Akizungumza na Mwanaspoti kocha huyo alisema kutolewa kwa timu hiyo katika Afcon kuna elimu kubwa wameipata.
Alieleza mambo mawili makubwa waliyoyapata kama makocha ambayo ni kwanza wachezaji wao wengi ni vijana hivyo wamekomaa kupitia mechi hizi tatu.
Alieleza kuwa la pili ni kwa wao kama makocha wamepata challenge ya kutakiwa kukisuka zaidi kikosi hasa eneo la ushambuliaji.
"Kama tungekuwa bora eneo la la kati kwenye ushambuliaji basi mechi hizi zisingekuwa na ugumu huu kwani zingekuwa ndani ya uwezo wetu na tungeziamua."
Usichokijua ni kwamba nchi zote tulizocheza nazo katika michuano hiyo kwa mara ya kwanza mwaka 1980, tumeshakwisha kuchezea viwanja vyake katika vipindi tofauti tofauti.