Straika wa Msuva aja Yanga
KIKOSI cha Yanga usiku wa jana kilikuwa uwanjani katika mechi yao ya mwisho ya michuano ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Namungo, lakini mabosi wao wanaendelea kukuna kichwa juu ya straika gani wamshushe kabla dirisha dogo halijafungwa ili kukamilisha hesabu zao.
Yanga wanataka kuleta straika atakayezitumia kwa ufasaha pasi tamu za Saido Ntibazonkiza kuitupia nyavuni, mezani kwao wana majina mawili, Mkongoman Idrisa Mbombo aliyepo Nkana ya Zambia na Mu-Ivory Coast, Gbagbo Junior Magbi anayekipiga na Simon Msuva ndani ya klabu ya Wydad Casablanca.
Mabosi wa Jangwani wanahaha kuhakikisha wanaingiza mashine moja ya kazi moja tu ya kufunga mabao ambayo itakuwa ni kama gia mpya kwao katika kuliwinda taji la ubingwa wa Simba ambao wanalishikilia kwa msimu wa tatu mfululizo.
Taarifa za uhakika ambazo Mwanaspoti halina shaka nazo ni kwamba mchakato wa usajili huo unafanyika chini ya matajiri wao GSM ambao sasa wanapiga hesabu za kupata jina moja kati ya Mbombo na Gbagbo ambaye ujio wa Msuva ndio uliomtibulia na sasa anataka kuondoka.
Yanga zilimpa kipaumbele Mbombo, ambaye alikubali kujua Jangwani, lakini utata bado upo katika dau lake la usajili ambalo alikuwa akitaka Dola 70,000 (zaidi ya Sh 160 milioni), wakati Yanga inataka kumpa 50,000 (Sh116 milioni), japo kwenye dau la mshahara alikuwa radhi kushusha kutoka dola 10,000 (kama Sh23 milioni), hata kutokana na du hilo, mabosi wa klabu hiyo wameamua kumgeukia Gbagbo ambaye ameonekana hana mambo mengi.
Hata hivyo, Yanga inatamani zaidi kumpata Mbombo kutokana na ubora wake akiwa chaguo lao la kwanza, lakini pia presha ya mastaa wa timu hiyo Tuisila Kisinda na Mukoko Tonombe waliowaambia mabosi wao kwamba jamaa ni mtu wa kazi wakimpoteza itawauma.
Wakongomani hao amemlainisha Mbombo na kukubali kushusha sehemu ya gharama hiyo ili aweze kuja Yanga ili waje kusaidiana kuipa mataji Yanga, lakini upande wa pili ni kwamba Gbagbo kwa sasa anasubiri majibu ya barua ya kuvunjiwa mkataba na Wydad ikubaliwe kama alivyoomba huku klabu yake wakitaka atolewe kwa mkopo.
Straika huyo yeye anachotaka avunjiwe mkataba kabisa ili wamalizane na kuachana na inaelezwa wakala wake tayari yupo Dar es Salaam ili kuweka mambo sawa, japo kuna ugumu kutoka kwa Rais wa Wydad, Said Naciri kama atakubali kumuachia kama mchezaji huru mshambuliaji huyo.
Hata hivyo, Muaivory Coast anaonekana kuwatia mzuka zaidi mabosi hao kuchekesha akili kuhakikisha wanambeba kama mipango yao itaenda sawa.
Kama Gbagbo atanaswa itaipa Yanga unafuu kupata mabao kwani kwa sasa wameongezewa mzuka kwa kutua Saido aliyefunga mabao mawili na kuasisti matatu katika mechi tatu tu.