Pigo Simba, Kajuna afariki Dunia
Muktasari:
- Kajuna amefariki alfajiri ya leo Julai 23, 2026 katika Hispitali ya Taifa Muhimbili kitengo cha Moyo baada ya kupumzishwa hapo kwa siku saba.
SIMBA imepokea taarifa ya simanzi baada ya kigogo wake mmoja wa Kamati ya Mashindano, Idd Kajuna kufariki dunia.
Kajuna amefariki alfajiri ya leo Julai 23, 2026 katika Hispitali ya Taifa Muhimbili kitengo cha Moyo baada ya kupumzishwa hapo kwa siku saba.
Mpaka anafariki, Kajuna alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Simba, ambapo pia amewahi kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Crescentius Magori, amethibitisha taarifa hiyo, akisema Simba imepoteza mpambanaji jasiri wa klabu hiyo.
Magori amesema Kajuna hakuwa tu kiongozi, bali alikuwa tayari wakati wote kuipigania Simba hata kabla ya kuteuliwa kwenye kamati hiyo.
"Hizi ni taarifa mbaya sana kwa Simba, tumepoteza mtu wa kupigana vitani, ni msiba mkubwa ndani ya Simba, alikuwa tayari wakati wote kuipambania Simba yake," amesema Magori.
"Unaweza kusema labda kwa sababu alikuwa kiongozi, lakini hapana, alikuwa anaipigania klabu hii hata kabla ya kuwa kiongozi na hilo ndilo likatufanya kumchagua kuwa Mjumbe wa Kamati ya Mashindano."
Taarifa zinasema, Kajuna atazikwa leo jioni Julai 23, 2026 kwenye makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam.