Straika Mkongomani atua Syria
Muktasari:
- Nyota huyo aliyejiunga na Singida Agosti 5, 2025, akitokea FC Saint-Eloi Lupopo ya kwao DR Congo, ametua Al-Fidaa SC baada ya kukosa nafasi kubwa ya kucheza mbele ya washambuliaji wengine wa Singida wakiongozwa na Jonathan Sowah na Mathew Momanyi Tegisi.
MSHAMBULIAJI wa Singida Black Stars raia wa DR Congo, Malanga Horso Mwaku amekamilisha uhamisho wake wa kujiunga na Homs Al-Fidaa SC ya Syria, kwa mkopo wa msimu mzima, baada ya dili lake la kujiunga na Pamba Jiji ya Mwanza kugonga mwamba.
Nyota huyo aliyejiunga na Singida Agosti 5, 2025, akitokea FC Saint-Eloi Lupopo ya kwao DR Congo, ametua Al-Fidaa SC baada ya kukosa nafasi kubwa ya kucheza mbele ya washambuliaji wengine wa Singida wakiongozwa na Jonathan Sowah na Mathew Momanyi Tegisi.
Mwaku aliyecheza pia timu ya Union Sportive Tshinkunku ya kwao DR Congo, tangu ajiunge na Singida Agosti 5, 2025, msimu wa 2025-2026, amehusika katika mabao matano ya Ligi Kuu Bara, baada ya kufunga manne na kutoa asisti moja.
Mshambuliaji huyo aliyesaini mkataba wa miaka mitatu na Singida, baada ya msimu huu wa 2026-2027 kumalizika maana yake atakuwa amebakisha mwaka mmoja, jambo linalomweka upya katika mazingira magumu ya kurejea tena ndani ya timu hiyo.
Sowah tayari ameendelea kuonyesha kiwango kizuri na timu hiyo baada ya kufunga mabao matatu ya Ligi Kuu Bara msimu huu wa 2026-2027, huku kwa upande wa Momanyi akifunga moja na wote wawili kuhusika na mabao manne kati ya 13, yaliyofungwa.