Metacha: Ushindani Singida Black Stars unanipa chachu
Muktasari:
- Kipa huyo mzawa amepita katika klabu sita tofauti nchini katika soka la ushindani, akizichezea Azam, Tanzania Prisons, Mbao FC, Yanga, Polisi Tanzania na sasa Singida Black Stars.
USHINDANI wa namba katika kikosi cha Singida Black Stars unampa presha kipa namba moja wa kikosi hicho, Metacha Boniphace Mnata ambaye amesema hata hivyo, badala ya kumkatisha tamaa, umekuwa chachu ya kuongeza juhudi na kuhakikisha kila mara anakuwa bora zaidi.
Kipa huyo mzawa amepita katika klabu sita tofauti nchini katika soka la ushindani, akizichezea Azam, Tanzania Prisons, Mbao FC, Yanga, Polisi Tanzania na sasa Singida Black Stars.
Metacha ambaye pia ni mlinda mlango wa Taifa Stars, amesema ushindani uliopo kwenye kikosi cha Singida Black Stars akiwania nafasi na Yona Amosi ni wa kujenga kwa sababu kila kipa anasukumwa kufanya vizuri zaidi, huku wakisaidiana kuhakikisha Singida inapata matokeo mazuri.
“Ushindani uliopo ni ushindani mzuri na wa kupambana ili klabu ifanye vizuri zaidi. Kwa hiyo ni vizuri kuwa nao. Tunapushiana mimi na yeye, tunasapotiana mimi na yeye,” amesema Metacha.
Amesema kuwa jambo la msingi katika ushindani huo ni kutoruhusu tofauti za kugombea namba kugeuka kuwa uhasama, badala yake kila mmoja anatakiwa kumuunga mkono mwenzake anapopewa nafasi ya kucheza.
“Yeyote atakayepata nafasi anapaswa kusapotiwa. Kama si mimi, basi acheze yeye; kama si yeye, basi nicheze mimi. Muhimu ni ushirikiano ili tufanye vizuri kwenye klabu,” amesema.
Metacha amesema pamoja na ushindani wa moja kwa moja wa nafasi ya kwanza, nidhamu na juhudi katika mazoezi ni miongoni mwa mambo yanayomsaidia kuendelea kupambana na kulinda nafasi yake.
“Kwanza ni nidhamu, pia ni juhudi kwenye mazoezi. Unapocheza mechi, unatakiwa kuhakikisha kila mechi unacheza uwe bora zaidi ya jana. Ukicheza kesho, unatakiwa kuwa bora zaidi ya mechi iliyopita,” amesema.
Metacha ndiye kipa namba moja wa Singida akifanikiwa kucheza mechi nne za Ligi Kuu Bara msimu huu akiwa na cleansheet moja huku akiruhusu mabao matano, wakati Yona Amosi aliyetua akitokea Pamba Jiji huku pia akiwahi kuitumikia Tanzania Prisons, amecheza mechi mbili bila cleansheet akiruhusu mabao manne.