MWENDELEZO wa kiwango anachokionyesha beki wa Yanga, Ibrahim Hamad ‘Bacca’, nyuma yake inatajwa nidhamu na bidii ya mazoezi, ndivyo vinavyompa heshima hadi sasa.
Mwanaspoti limezungumza na wachezaji wenzake, ambao wamezungumzia namna ambavyo anajituma na kulinda kiwango chake, jambo ambalo linamfanya kila kocha ajaye kumtumia kwenye kikosi cha kwanza.
Ingawa hakuanza moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza baada ya kusajiliwa Yanga katika dirisha dogo la msimu wa 2021/22 akitokea KMKM ya Zanzibar ambako alizichezea pia timu nyingine kama Malindi na Jang’ombe Boys, aliwahi kufanya mahojiano na Mwanaspoti na kuelezea jinsi ambavyo alivumilia hadi ulipofika muda wa kupewa nafasi ya kucheza.
“Nakumbuka kocha Nasreddine Nabi alimtuma msaidizi wake, Cedrick Kaze, aniambie nitaanza mechi dhidi ya KMC. Hiyo ndiyo ilikuwa mechi yangu ya kwanza. Nikaingia chumbani, nikapiga goti na kumuomba Mungu anitangulie, anipe utulivu ili nisicheze kwa papara nikajikuta nakosea. Ilipofika siku ya mechi nilifanya vizuri, tangu hapo nikaanza kuaminiwa,” anasema.
Kiwango cha Bacca kimeendelea kupanda, licha ya Yanga kusajili wachezaji katika nafasi anayocheza kama Mamadou Doumbia, aliyetokea Stade Malien, Gift Fred (Villa ya Uganda), ambao walijiunga na Wanajangwani hao msimu wa 2023/2024 na Frank Assinki msimu wa 2025/26, akitokea Singida Black Stars. Wote hao hakuna aliyemuweka benchi beki huyo.
Ukiachana na hilo, Bacca siyo mchezaji wa kupata majeraha ya mara kwa mara na ya muda mrefu. Inapotokea anakaa nje ya uwanja, sababu inakuwa ni adhabu za kadi, jambo ambalo wachezaji wenzake wanalizungumzia kuwa linatokana na nidhamu na kujitunza.
Beki wa zamani wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, anasema: “Ukimuona mchezaji amecheza kwa muda mrefu katika klabu za Yanga na Simba, kwanza ana nidhamu, anajitunza na ana bidii ya kufanya mazoezi. Hayo ndiyo anayoyafanya Bacca, ni mtu aliye na bidii na anayezingatia miiko ya kazi yake.”
Anaongeza: “Bacca anapenda kuzingatia muda na kupumzika, siyo mchezaji wa kuzurula mtaani. Naamini hayo yanamsaidia acheze kwa kiwango cha juu hadi sasa.”
Mwingine aliyemzungumzia hilo ni golikipa wa Yanga, Hussein Masalanga: “Bacca ana nidhamu ya muda, kwa maana kila kitu anakifanya kulingana na wakati unaotakiwa. Mfano, kulala kwa wakati, kula kwa wakati, kufika mazoezini kwa wakati. Siyo mchezaji wa kujivutavuta kufanya vitu, labda inatokana pia na kazi ya askari.”
Hata baada ya kuondoka kwa kocha Nabi, ambaye alimpa nafasi ya kuonyesha kiwango chake baada ya kuinoa Yanga kuanzia 2021–2023, bado makocha wengine waliopita katika timu hiyo waliendelea kumtumia Bacca katika kikosi cha kwanza.
Makocha hao ni Miguel Gamondi (2023/24), Sead Ramovic (2024–2025), Miloud Hamdi (2025), Romain Folz (2025), Pedro Goncalves (2025) na Manqoba Mngqithi (2026/27), ambao walitengeneza pacha baina ya Bacca na Dickson Job.
Jambo ambalo aliyekuwa kocha wa Simba, Fadlu Davids, ambaye aliwahi kuitaka huduma yake wakati anaifundisha Raja Casablanca ya Morocco, anasema: “Bacca ni beki mzuri, ana utulivu, anajua kwenda na muda wa kwenda kuokoa hatari wakati mpira unaelekezwa golini kwao. Hakuna kocha anayeweza kuacha kumtumia.”
Katika timu ya Taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’, Bacca amecheza jumla ya mechi 37 na kufunga bao moja. Ingawa katika nafasi hiyo kuna ushindani mkali, bado anapata nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza.
Miongoni mwa mechi ambazo alifanya vizuri akiwa na Taifa Stars ni dhidi ya Guinea iliyopigwa Novemba 19, 2024. Bacca alimzuia Serhou Guirassy na Stars ikapata ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Simon Msuva, likaisaidia timu kufuzu kucheza fainali za AFCON.
Staa wa zamani wa Taifa Stars, Erasto Nyoni aliyeichezea timu hiyo kuanzia 2006 hadi 2021, alicheza mechi 107 na kufunga mabao saba anasema: “Timu ya taifa ina wachezaji wengi, ukiona mchezaji anaitwa mara kwa mara na anacheza, basi anajitunza na anafanya sana mazoezi. Mpira wa miguu unachezwa sehemu ya wazi, hivyo mchezaji kiwango kikiwa juu kinaonekana, pia akicheza chini ya kiwango anaonekana.”
Kapteni (N) Hussein Ali Makame, ambaye ni Mkuu wa Teknolojia na Michezo wa KMKM, ambao ndio waajiri wa Bacca katika kazi ya uaskari, anasema: “Nidhamu ya Bacca inachangia na kazi yake ya askari, kwani tunasisitiza awe mfano kila sehemu anapokuwepo. Nikiri, tunatambua ana nidhamu ya juu ndiyo maana anafanikiwa.”