Straika apotezea kiatu cha ufungaji bora
Muktasari:
- Mshambuliaji huyo amejiunga na timu hiyo baada ya msimu wa 2025-2026, kuichezea African Sports ya jijini, Tanga kisha dirisha dogo la Januari 2026, akajiunga na B19 FC kwa sasa Kigamboni United FC, aliyomaliza kwa kuifungia mabao matano.
MSHAMBULIAJI wa maafande wa Transit Camp, Hamdan Sarhani amesema licha ya kiwango kizuri anachoendelea kukionyesha hadi sasa katika Ligi ya Championship, ila malengo yake ya kufunga mabao ameivunja na haangalii tena suala la ufungaji bora.
Akizungumza na Mwanaspoti, Sarhani amesema malengo yake ya raundi ya kwanza yalikuwa ni kufikisha mabao manane, ingawa tayari rekodi hiyo ameivunja na sasa anaendelea kupambana zaidi kwa ajili ya kukipigania kikosi hicho cha Transit Camp.
“Sitaki kuzungumzia suala la ufungaji bora kwa sasa, ila ikitokea nitashukuru kwa sababu malengo ni kuona naendelea pia kufanya vizuri kwa ajili ya timu na kwangu binafsi, nashukuru kwa hatua kubwa niliyoifikia msimu huu,” amesema Sarhani.
Nyota huyo aliyeanzia JKT Tanzania na baadaye kujiunga na timu za vijana za Simba, ndiye anayeongoza katika ufungaji kwa msimu huu, baada ya kufunga mabao 12, nyuma ya mshambuliaji wa kikosi cha KMC, Ramadhan Hashim Kalanje aliyefunga tisa.
Mshambuliaji huyo amejiunga na timu hiyo baada ya msimu wa 2025-2026, kuichezea African Sports ya jijini, Tanga kisha dirisha dogo la Januari 2026, akajiunga na B19 FC kwa sasa Kigamboni United FC, aliyomaliza kwa kuifungia mabao matano.