Simba yaivaa TFF sakata la uchaguzi mkuu
Muktasari:
- Katika taarifa yake iliyotolewa leo, Novemba 15, 2026, Simba imesema imesikitishwa na kauli zilizotolewa hadharani kuhusu uchaguzi wake, huku ikisisitiza kuwa klabu hiyo ni taasisi moja na haina pande mbili kama ilivyodaiwa.
MVUTANO unaoendelea kuhusiana na mwenendo wa Uchaguzi Mkuu wa Simba umechukua sura mpya baada ya Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo kujibu hadharani kauli zilizotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wakili Kiomoni Kibamba.
Katika taarifa yake iliyotolewa leo, Novemba 15, 2026, Simba imesema imesikitishwa na kauli zilizotolewa hadharani kuhusu uchaguzi wake, huku ikisisitiza kuwa klabu hiyo ni taasisi moja na haina pande mbili kama ilivyodaiwa.
Bodi ya Wakurugenzi ya Simba imesema tayari klabu hiyo ilikuwa imeiandikia TFF barua rasmi Novemba 13, 2026, ikieleza msimamo wake kuhusu mwenendo wa mchakato wa uchaguzi, ikitoa mapendekezo ya kuboresha na kuomba majibu rasmi kwa maandishi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Simba haikuridhishwa na hatua ya baadhi ya viongozi wa chombo kinachosimamia mpira wa miguu kutoa maelezo kwa vyombo vya habari kabla ya kuijibu klabu rasmi kwa maandishi.
“Klabu inaona si sahihi kwa kiongozi wa chombo kinachosimamia mpira wa miguu kujibu barua rasmi ya klabu kupitia vyombo vya habari kabla ya kuipa klabu majibu ya maandishi,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Katika moja ya hoja zilizosisitizwa, Simba imepinga kauli iliyoielezea klabu hiyo kama yenye pande mbili zinazopingana, zikitajwa kuwa na ofisi tofauti za Masaki na Msimbazi.
Simba imesema kauli hiyo si sahihi na inaweza kuzua mkanganyiko miongoni mwa wanachama, mashabiki na wadau wake, huku ikisisitiza kuwa klabu inaongozwa kwa Katiba moja.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Katiba ya Simba ya mwaka 2018, iliyofanyiwa marekebisho Novemba 30, 2025 na kusajiliwa Februari 18, 2026, ndiyo inayosimamia shughuli za klabu hiyo.
“Kila mwanachama, shabiki, mdhamini, mchezaji, kocha na mfanyakazi wa klabu atambue kuwa Simba ni moja,” imeeleza taarifa hiyo.
Licha ya hayo yote, Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo imesema Simba inaendelea kusisitiza dhamira yake ya kuhakikisha uchaguzi wake unafanyika kwa uhuru, haki, uwazi na kwa kuzingatia kanuni na taratibu husika.
Imesema uchaguzi unapaswa kuongozwa kwa mujibu wa Katiba ya Simba, Kanuni za Uchaguzi pamoja na kanuni za TFF na FIFA, huku ikisisitiza umuhimu wa kuheshimiana na kuelewana katika kipindi hiki muhimu.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, jopo la wanasheria wa klabu linaendelea kutathmini hatua zaidi za kisheria kufuatia kauli zilizotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
Wakati suala hilo likiendelea, Simba imewataka wanachama, mashabiki na washirika wake kubaki watulivu na kudumisha umoja.
“Tunawaomba wanachama, mashabiki na washirika wetu wote kuendelea kuwa watulivu na wamoja,” imeeleza taarifa hiyo.
Januari 30, 2026, Klabu ya Simba inatarajiwa kufanya uchaguzi mkuu wa kupata viongozi wapya baada ya wale waliopo madarakani muda wao kuelekea ukingoni. Kamati ya Uchaguzi ya TFF ndiyo itasimamia mchakato mzima.
Katika uchaguzi huo ambao kesho Jumatatu Novemba 16, 2026 zoezi la kutoa na kurejesha fomu linaanza, kuna nafasi moja ya mwenyekiti inagombewa, huku wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi zikiwa nafasi tano.