KMC yaonja jiwe la joto baada ya dakika 810
Muktasari:
- KMC imepoteza mchezo wake wa kwanza katika Championship ikilala mbele ya Prisons, huku straika Oscar Paul akiendelea kutakata katika ligi hiyo akifunga kwenye mechi tatu mfululizo.
Baada ya kucheza mechi tisa mfululizo bila kupoteza, hatimaye KMC imeonja uchungu wa Ligi ya Championship kufuatia kukutana na kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons.
Matokeo hayo yanaifanya KMC kushuka kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo hadi nafasi ya tatu kwa pointi 19, huku Prisons ikipanda nafasi ya pili kwa pointi 20, wakati Mtibwa Sugar ikishikilia usukani kwa pointi 21.
Mbali na hilo, straika wa Prisons, Oscar Paul ameendelea kuwa mwiba katika Championship kutokana na kasi ya kufunga mabao akifanya hivyo mechi tatu mfululizo akifikisha saba, nyuma ya kinara Hamdan Ally wa Transit Camp mwenye 12.
Prisons iliyoshuka daraja msimu uliopita kupitia play off, inakuwa ya kwanza kuisimamisha KMC na kuendelea kujipa matumaini ya kurudi Ligi Kuu kufuatia matokeo iliyonayo.
Katika mchezo wa leo Novemba 15, 2026 uliopigwa uwanja wa Sokoine, Mbeya, licha ya ushindani na ubora wa timu zote, wenyeji walipata bao dakika ya 53 kupitia Paul.
Baada ya mchezo huo, Prisons inatarajia kurejea uwanjani wikiendi ijayo kuwafuata ndugu zao KenGold huko wilayani Chunya mkoani Mbeya, huku KMC ikiwa mgeni mbele ya TMA huko mkoani Iringa.
Straika wa KMC, Ramadan Kalanje, amesema kupoteza mchezo huo ni sehemu ya matokeo ya mpira, akieleza kuwa kwa sasa wanajiandaa tena na mechi inayofuata kuhakikisha wanarejesha ubora wao.
"Hatujapoteza mwelekeo, malengo ni kurudi Ligi Kuu, matokeo ya leo ni sehemu ya mpira, tulijua ugumu wake lakini tutajipanga, binafsi nahitaji kuwa kinara wa mabao na kuipandisha timu," amesema nyota huyo mwenye mabao tisa.
Kwa upande wake straika wa Prisons, Oscar Paul amesema mafanikio yao ni kufuata maelekezo ya benchi la ufundi akieleza kuwa kiu yao ni kuona timu inarejea tena Ligi Kuu.
"Kwanza malengo ni kuipa mafanikio timu, kiu kubwa ni kuona Prisons inarejea Ligi Kuu, sababu ya mafanikio ni utekelezaji wa maelekezo ya benchi la ufundi ingawa bado ligi ni ngumu," amesema.