Sowah kama alivyoanza Simba
Muktasari:
- Sowah aliyerejea Singida Black Stars Julai 15, 2026, akitokea Simba aliyoitumikia kwa msimu wa 2025-2026, amefunga bao hilo Agosti 14, 2026 dhidi ya Fountain Gate, ikiwa ni kama pia alivyofanya akikitumikia kikosi hicho cha Msimbazi.
MSHAMBULIAJI wa Singida Black Stars, Jonathan Sowah ameanza maisha yake mapya na kikosi hicho kama ilivyokuwa na Simba, baada ya kuifungia timu hiyo bao moja la Ligi Kuu Bara, katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Fountain Gate.
Sowah aliyerejea Singida Black Stars Julai 15, 2026, akitokea Simba aliyoitumikia kwa msimu wa 2025-2026, amefunga bao hilo Agosti 14, 2026 dhidi ya Fountain Gate, ikiwa ni kama pia alivyofanya akikitumikia kikosi hicho cha Msimbazi.
Bao lake la kwanza la Ligi Kuu Bara msimu wa 2025-2026, aliifungia Simba katika ushindi wa kikosi hicho wa mabao 3-0 dhidi ya Fountain Gate, Septemba 25, 2025, jambo ambalo amelirudia akiwa na Singida Black Stars, Agosti 14, 2026.
Mechi ya Septemba 25, 2025, Sowah aliifungia Simba bao moja la dakika ya 57, huku mengine yakifungwa na beki wa kati, Rushine De Reuck dakika ya tano na aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Jean Charles Ahoua dakika ya 36.
Kwa msimu huu wa 2026-2027, Sowah ameifungia Singida bao moja la dakika ya 28, huku mengine yakifungwa na Yusuph Khamis dakika ya 81 na Mathew Momanyi dakika ya 90+4 na kuiwezesha timu hiyo kushinda pia mabao 3-0 dhidi ya Fountain Gate.
Mshambuliaji huyo raia wa Ghana, licha ya kutabiriwa makubwa na kikosi hicho cha Msimbazi kwa msimu wa 2025-2026, lakini alishindwa kuwika kutokana na sababu mbalimbali za nje ya uwanja, alimaliza kwa kufunga mabao matatu ya Ligi Kuu.
Sowah aliyejiunga na Singida Black Stars akitokea Al-Nasr Benghazi SC ya Libya.