Kocha: Sowah atawashangaza
Muktasari:
- Sowah, aliyerejea Singida Black Stars dirisha hili la usajili, ameanza tena kuitumikia timu hiyo katika michuano ya Kagame Cup huku akibeba matumaini makubwa ya kuiongoza safu ya ushambuliaji kuelekea msimu mpya wa 2026-2027.
LICHA ya Singida Black Stars kuanza vibaya kampeni ya kutetea ubingwa wa CECAFA Kagame Cup 2026 kwa kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Jamus SC ya Sudan Kusini, kocha wa timu hiyo, Papy Kimoto, amewataka mashabiki kutokuwa na hofu akiamini mshambuliaji wa Ghana, Jonathan Sowah, ataonyesha makali yake kadri mashindano yanavyoendelea.
Sowah, aliyerejea Singida Black Stars dirisha hili la usajili, ameanza tena kuitumikia timu hiyo katika michuano ya Kagame Cup huku akibeba matumaini makubwa ya kuiongoza safu ya ushambuliaji kuelekea msimu mpya wa 2026-2027.
Mshambuliaji huyo aliwahi kung’ara akiwa na Singida kwa kufunga mabao 13 katika msimu wake wa kwanza wa Ligi Kuu Bara 2024-2025, kiwango kilichoisukuma Simba SC kumsajili mwanzoni mwa msimu wa 2025-2026.
Hata hivyo, maisha yake Msimbazi hayakwenda kama ilivyotarajiwa baada ya kusimamishwa kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni utovu wa nidhamu, alidumu msimu mmoja pekee, Julai 2026 akarejea Singida.
Katika mchezo dhidi ya Jamus SC, Kimoto alifanya mabadiliko kadhaa kipindi cha pili akimwingiza Sowah kwa lengo la kuongeza nguvu safu ya ushambuliaji.
Mghana huyo pamoja na Linda Mtange walitengeneza nafasi kadhaa lakini walishindwa kuzitumia na Singida ikaondoka mikono mitupu.
Licha ya matokeo hayo, Kimoto amesema ana imani kubwa na Sowah, akieleza mshambuliaji huyo anahitaji muda mfupi kurejea kwenye ubora wake na anaamini atakuwa silaha muhimu kwa Singida katika mashindano hayo na msimu ujao.
“Sowah ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa. Ameanza kurejea kwenye kiwango chake na ninaamini atatusaidia sana,” amesema Kimoto.
Singida Black Stars na Simba SC zinatumia Kagame Cup kama sehemu ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa huku kila timu ikitumia mashindano hayo kupima uimara wa vikosi vyao.