Simba yazidi kutakata
Wakati Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck akitaka ushindi wa ugenini katika mechi yao ya keshokuwa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, meneja wa timu hiyo, Abbas Ali ameweka wazi hali ya wachezaji na namna wanavyoishi tangu walipowasili nchini Zimbabwe.
Simba iko mjini Harare kwa siku kadhaa sasa ikiendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Alexandra Sports Club, ikijiandaa kuikabili Platinum, Jumatano, mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa National Sports kuanzia saa 10 jioni kwa Tanzania na saa 9 Alasiri kwa saa za Zimbabwe
Juzi, kocha Sven alikuwa na programu ya mazoezi ya asubuhi na jana ilifanya mazoezi ya jioni pekee huku akisisitiza kutaka ushindi wa ugenini.
“Timu iko vizuri, kila mchezaji ana ari ya ushindi na bila shaka tutafanya vizuri na kushinda ugenini kwani ndiyo malengo ya kila mmoja wetu,” alisema kocha huyo.
Akizungumzia maisha yao tangu wamewasili Harare, meneja wa Simba, Ali alisema katika kipindi chote ambacho wapo nchini humo wamekuwa katika hali ya utulivu kambini.
“Tukitoka hotelini ni mazoezini na kurudi hotelini basi, huo ndiyo utaratibu wetu tangu tumewasili.Hapa Harare wako kwenye changamoto ya janga la corona, hivyo hakuna purukushani zozote hata za mashabiki wa wapinzani wetu kuelekea kwenye mechi hii, hali ni ya utulivu,” alisema.
Simba imepiga kambi kwenye hoteli ya nyota tatu ya Cresta Lodge kujiandaa na mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kushinda ile ya awali dhidi ya Plateau United ya Nigeria.
Simba itaikabili Platinum ikiwa na rekodi nzuri katika mechi tano za mwisho kulinganisha na wapinzani wao, ambao wamefungwa mbili na kushinda mbili, huku ikitoka sare ya 1-1 na Al Ahly nyumbani.
Simba imekuwa na matokea ya ushindi wa tabu katika Ligi Kuu, lakini nyongeza ya nyota wa Thadeo Lwanga inafanya eneo la kiungo kuimarika na kuongeza imani katika mechi zijazo.
Lwanga hajaichezea Simba bado lakini amesafiri na timu nchini Zimbabwe kwa ajili ya mchezo huo.