Simba yatesti mitambo ya CAF

VINARA wa Ligi Kuu Bara na wawakilishi wa Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba jioni ya leo watatesti mitambo ya CAF, itakapovaana na Asante Kotoko ya Ghana kwenye mechi ya michuano maalumu iliyoandaliwa na Al Hilal ya Sudan ili kujiandaa na michuano ya kimataifa.
Al Hilal imeandaa michuano hiyo inayoshirikisha timu tatu na Simba inatupa karata yake ya kwanza saa 10:00 jioni kuvaana na Asante Kotoko ambayo juzi usiku ilipasuliwa na wenyeji wa michuano hiyo kwa mabao 5-0.
Kocha Zoran Maki anataka kuzitumia mechi hizo kunoa makali ya timu hiyo kabla ya kuanza mbio za michuano ya kimataifa inayoanza mwezi ujao, Simba ikipangwa kuanzia raundi ya kwanza ikipangwa kucheza na Nyasa Big Bullets ya Malawi.
Simba iliondoka na wachezaji 18 kwa ajili ya michuano hiyo kutokana na wachezaji wake tisa wakiwamo makipa Aishi Manula na Beno Kakolanya kuwa kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars ambayo jioni ya leo inashuka uwanjani kuvaana na Uganda kwenye mechi ya kuwania Fainali za CHAN 2023.
Wengine waliopo Stars ni; Mzamiru Yasin, Shomary Kapombe, Jonas Mkude, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Kennedy Juma, Kibu Denis na Habib Kyombo. Sadio Kanoute na Joash Onyango ni wachezaji wengine waliokwamba kuambatana na timu nchini Sudan kwa sababu mbalimbali.
Onyango amebaki jijini Dar kutokana na kutoridhishwa kuwekwa benchi na Kocha Maki, wakati Kanoute amekwamishwa na ishu za hati (visa) ya kumruhusu kuingia Sudan.
Licha ya kuwakosa wachezaji hao, lakini kocha Maki alisema anaamini vijana alioenda nao Sudan
kupitia mechi hizo watampa mwanga mzuri wa maandalizi ya mechi zilizo mbele yao ikiwamo ya Ligi Kuu dhidi ya KMC itakayopigwa Septemba 7 kabla ya kusafiri kwenda Malawi kucheza na Nyasa.
Maki alisema wachezaji waliopo Stars kwa vile watakuwa wanacheza, itawasaidia kuwa fiti na hata atakapoungana nao kwenye safari ya kwenda Malawi bado hawatatofautiana na wenzao ambao baada ya mechi ya leo dhidi ya Waghana, Jumanne watarudi tena uwanjani kucheza na wenyeji Al Hilal katika mechi ya kisasi kwani Januari mwaka jana katika michuano kama hiyo iliyoandaliwa na Simba na kupewa jina la Simba Super Cup, Wasudan walifumuliwa mabao 4-1 Kwa Mkapa.
Katika mechi hiyo ya mwaka jana, Simba ilipata mabao yake kupitia Rally Bwalya aliyefunga dakika ya 39 kabla ya Jamal Salim kuisawazishia Al Hilal dakika ya 45, kisha Perfect Chikwende kufunga bao la pili dakika ya 72 na Bernard Morrison alimalizia kwa kufunga mawili dakika ya 87 na 90.
Michuano hiyo ya Simba Super Cup 2021 ilishirikisha pia TP Mazembe ya DR Congo ambayo ilicheza na Simba mechi ya kufungia pazia la michuano hiyo na pambano kumalizika kwa suluhu.
Mara Simba itakapocheza na Al Hilal itarejea jijini Dar es Salaam kwa mchezo mwingine wa kutesti mitambo ya CAF kwa kuvaana na AS Arta Solar 7 ya Djibouti itakayopigwa Septemba 3 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ndipo siku nne baadaye kuivaa KMC katika mechi ya Ligi Kuu Bara.