Rayon Sports yatwaa ubingwa wa Kagame baada ya miaka 28
Muktasari:
- Ushindi huo umeifanya Rayon Sports kutwaa ubingwa wake wa pili katika historia ya mashindano hayo, baada ya miaka 28 kupita kwani mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1998 ilipoifunga Mlandege FC ya Zanzibar mabao 2-1, huko Zanzibar.
RAYON Sports ya Rwanda, imetwaa ubingwa wa Kombe la CECAFA Kagame 2026 baada ya kuichapa Gor Mahia ya Kenya mabao 2-1 ndani ya dakika 120 katika mchezo wa fainali uliopigwa leo Ijumaa Agosti 7, 2026 kwenye Uwanja wa Amahoro hapa Rwanda.
Ushindi huo umeifanya Rayon Sports kutwaa ubingwa wake wa pili katika historia ya mashindano hayo, baada ya miaka 28 kupita kwani mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1998 ilipoifunga Mlandege FC ya Zanzibar mabao 2-1, huko Zanzibar.
Kwa upande wa Gor Mahia, ilishindwa kuongeza idadi ya mataji yake matatu ya CECAFA iliyoyatwaa mwaka 1980, 1981 na 1985 ilipotwaa ubingwa huo kwa mara ya mwisho jijini Khartoum nchini Sudan.
Mbele ya maelfu ya mashabiki waliofurika Uwanja wa Amahoro, Rayon Sports ilianza mchezo kwa kasi, ikitawala umiliki wa mpira na kuonyesha wazi dhamira ya kupata bao la mapema huku ikitumia vyema faida ya kucheza nyumbani.
Presha hiyo ya mashambulizi ilizaa matunda ndani ya dakika 30 za kwanza baada ya Junior Kameni kufunga bao la kuongoza kufuatia piga nikupige.
Baada ya bao hilo, Gor Mahia ilijaribu kujibu kwa mashambulizi ya kushtukiza, lakini safu ya ulinzi ya Rayon ilisimama imara na kuhakikisha wenyeji wanaenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili kilianza huku Rayon Sports ikionekana kubadili mbinu na kucheza kwa tahadhari zaidi, ikilinda bao lake huku ikiwapa nafasi wageni kushambulia zaidi.
Gor Mahia iliongeza kasi ya mchezo na hatimaye juhudi zao zikazaa matunda dakika ya 54, Shariff Musa alipoifungia timu hiyo bao la kusawazisha na kurejesha matumaini ya kutwaa ubingwa.
Bao hilo lilibadilisha kabisa sura ya mchezo, kwani Rayon Sports iliacha kucheza kwa kujihami na kuanza kushambulia tena, hali iliyofanya timu hizo kushambuliana kwa zamu.
Licha ya juhudi hizo, dakika 90 za muda wa kawaida zilimalizika kwa sare ya bao 1-1 na kulazimisha kuchezwa kwa dakika 30 za nyongeza ili kumpata bingwa.
Katika dakika ya 98 ya muda wa nyongeza, Muhoza Daniel aliibuka shujaa wa Rayon Sports baada ya kufunga bao la pili na kuiweka timu hiyo mbele kwa mabao 2-1.
Gor Mahia ilifanya kila juhudi kusaka bao la kusawazisha katika dakika zilizobaki, lakini safu ya ulinzi ya Rayon Sports ilikuwa imara hadi filimbi ya mwisho ilipopulizwa.
Kwa ushindi huo, Rayon Sports imeondoka na kitita cha dola 30,000 (Sh79.5 milioni) kama mabingwa wa CECAFA Kagame 2026 huku Gor Mahia ikiambulia dola 20,000 (Sh53 milioni) kwa kumaliza katika nafasi ya pili.