Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba yapiga mkwara, Robertinho apata mifumo mitatu ya mauaji

SIMBA imefunga kambi ya mazoezi kwa kucheza mechi ya mwisho ya kirafiki juzi jioni dhidi ya Batman Petrolspor A.S na leo imeanza safari ya kurejea nchini kujiandaa na mechi ya Simba Day kisha kwenda Tanga kwenye Ngao ya Jamii, huku benchi la timu hiyo likichimba mkwara mzito.

Mechi hiyo ilikuwa ni ya nne kwa Simba baada ya awali kucheza na Zira na kutoka sare ya 1-1 kisha kucheza na Turan PFK na kuifunga 2-0 kabla ya kukubali kipigo cha 1-0 kwa timu hiyo hiyo na jana ilikuwa inacheza mechi ya nne na kocha wa timu hiyo, Roberto Oliveira 'Robertinho' akasema kwa kujiamini kwamba chama limeiva na wapinzani wajiandae kwani wataumia mbele yao.

Robertinho alisema anapata jeuri ya kuchimba mkwara huo kutokana na kuringia mastaa alionao nao ambao wameisuuza roho yake na kumpa mifumo mitatu ya kumbeba aksisitiza safari hii heshima inarudi Msimbazi.

Kocha huyo raia wa Brazili aliliambia Mwanaspoti kuwa kambi yao ya Uturuki imekuwa na manufaa makubwa kwani na sasa amepata mifumo mitatu ambayo Simba inaweza kutumia katika michuano yote kwa msimu unaoanza mwezi ujao.

Robertinho alisema mifumo hiyo imetokana na upana wa kikosi chake kufuatia ujio wa mastaa bora ambao wamekuja na nguvu kubwa kuunganisha na wale ambao wamewakuta.

"Tumekuwa na wakati mzuri hapa Uturuki, nimeridhika na kazi ambayo imefanyika hapa kwa kuwaandaa wachezaji na sasa tunarudi kuendelea na maandalizi mengine, unajua huwezi kusema hizi wiki tatu zimetosha kukamilisha kila kitu," alisema Robertinho na kuongeza;

"Nimefurahia ubora wa wachezaji wapya, hapa niwaambie mashabiki wa Simba kwamba timu tunayo, wachezaji wote wapya kuna kitu wametuonyesha kikubwa sasa tunaweza kubadili mifumo ya uchezaji hata mara tatu itategemea na ubora wa wapinzani tutakaokutana nao."

Hata hivyo kocha huyo alikataa kuanika mifumo hiyo kwa kusema ni sawa na kuuza siri za kambi ya vita, lakini akasema ataitesti kwenye mechi ya Tamasha la Simba Day dhidi ya Wazambia Power Dynamos kabla ya kuhamishia kwenye Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba itacheza na Dynamos, Jumapili hii kisha Alhamisi itavaana na Singida Fountain Gate katika mechi ya Ngao ya Jamii jijini Tanga na baadae kujiandaa na Ligi Kuu Bara inayoanza Agosti 15.

"Tunataka kupambana kuhakikisha muunganiko huu unakamilika haraka kwa hili kundi la wachezaji wapya na wenzao ambao wamewakuta, tuna muda mfupi lakini sasa ni wakati wa kufanya sana kazi kati yetu makocha na wachezaji ili tufikie malengo ya msimu ujao," alisema Robertinho.

Akizungumzia kufungwa kwa idadi ya mabao machache katika mechi zao za kirafiki Robertinho alisema hilo wala halimpi wasiwasi kwani itakapokamilika kazi ya kuwaunganisha wachezaji wake kisha wakaelewana mabao mengi yatakuja.

"Unajua kwanza tulikuwa tunapambana kuimarisha miili yao hili lilikuwa muhimu sana na tumeridhika kwamba hilo limekamilika vizuri kazi ambayo tuliianza hii wiki ya mwisho ni kuangalia namna gani wataunganika na kuelewana.

"Inahitaji muda jambo zuri tunatengeneza nafasi, tukiongeza nguvu kidogo wachezaji wangu watakuwa wameelewana na hapo ndipo mabao zaidi yatafungwa, nina furahja kuona wachezaji wenyewe wana kiu ya mafanikio.

"Kama mmeona asilimia kubwa ya mabao yamefungwa na wachezaji ambao wanajuana na waliwahi kufika hapa kuna wengine walichelewa kufika hapa wanahitaji muda hilo sio tatizo kabisa."