Chama la Wana mguu sawa Championship
Muktasari:
- Imesema kutokana na nguvu ya wadau, mashabiki na uimara wa uongozi, watashirikiana kwa pamoja kukamilisha mipango yote kwa siku tano na kujiweka tayari na ligi hiyo msimu ujao.
STAND United ‘Chama la Wana’ imesema licha ya kuchelewa kufanya usajili, lakini inaamini hadi Jumatatu ya wiki ijayo itakuwa imekamilisha kila kitu na timu kuanza kambi ya kujiandaa na Ligi ya Championship msimu ujao 2026-2027.
Imesema kutokana na nguvu ya wadau, mashabiki na uimara wa uongozi, watashirikiana kwa pamoja kukamilisha mipango yote kwa siku tano na kujiweka tayari na ligi hiyo msimu ujao.
Timu hiyo ya mjini Shinyanga, iliwahi kushiriki Ligi Kuu kabla ya kushuka daraja na sasa ipo Ligi ya Championship na msimu uliopita haikuwa na matokeo mazuri iliposubiri matokeo ya mchujo ‘play off’.
Katibu Mkuu wa Stand United, Fredy Masai amesema sababu ya kuchelewa kufanya usajili ni kutokana na masuala ya kifedha yaliyokuwa yanaipa wakati mgumu tangu msimu uliopita, jambo ambalo limepata muafaka.
Amesema kurudi kwa baadhi ya waliokuwa viongozi na Jambo ambaye ni mdau mkubwa wa timu hiyo mjini Shinyanga kwa kuamua kutoa sapoti, ni hatua kubwa katika kufanikisha mipango kwa ajili ya msimu ujao.
“Msimu uliopita haukuwa mzuri kwetu lakini sababu kubwa ilikuwa ni fedha, hivyo katika kikao cha Julai 27 tuliazimia kuirudisha timu katika ubora kwa kila mmoja kuichangia ili tuondokane na presha.
“Kuna mdau wetu Jambo ameamua kutushika sehemu na mashabiki kulipia kadi za uanachama na baadhi ya waliokuwa viongozi wameamua kurudi kwenye timu, hivyo nguvu zote hizo zitatufikisha pazuri,” amesema Masai.
Ameongeza mipango ya timu hiyo inaanza leo (jana) kwa kamati kukutana kuanza kujadili usajili na maboresho kwenye eneo la benchi la ufundi kwa ajili ya kuanza kambi rasmi.
“Kambi itaanza Jumatatu ijayo, naamini kuanzia vikao vyetu leo tutaanza kusajili wachezaji, kutokana na muda hatutakuwa na majaribio badala yake tunahitaji wale wa kuja kucheza kutupa matokeo” amesema Katibu huyo.