Marcel Canadi; Ndoto ya CAF na Changamoto Mpya Singida Black Stars
Muktasari:
- Mchezaji huyo mwenye asili ya Austria ametua Singida Black Stars akiwa na historia ya kucheza soka la kiwango cha juu barani Ulaya, ikiwemo kupitia mfumo wa soka wa Austria na Ujerumani, jambo lililomfanya baadhi ya mashabiki kumpachika jina la “Mzungu wa Bundesliga” kutokana na uzoefu wake katika mazingira ya soka la Ulaya.
SINGIDA Black Stars imekuwa miongoni mwa klabu zilizotikisa katika dirisha la usajili kuelekea msimu wa 2026/27, miongoni mwa wachezaji hao ni pamoja na kiungo mshambuliaji Marcel Canadi.
Mchezaji huyo mwenye asili ya Austria ametua Singida Black Stars akiwa na historia ya kucheza soka la kiwango cha juu barani Ulaya, ikiwemo kupitia mfumo wa soka wa Austria na Ujerumani, jambo lililomfanya baadhi ya mashabiki kumpachika jina la “Mzungu wa Bundesliga” kutokana na uzoefu wake katika mazingira ya soka la Ulaya.
Ni mchezaji mwenye jukumu kubwa la kuongeza ubunifu katika safu ya ushambuliaji ya Singida Black Stars, ambayo msimu ujao itapambana katika Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la CRDB na Kombe la Shirikisho Afrika.
Mwanaspoti tukuwa Kigali, Rwanda kwa ajili ya kukujuza kila ambacho kinaendelea katika maandalizi ya klabu za Tanzania, tulipata nafasi ya kufanya naye mahojiano maalum ambapo ameeleza kuwa Tanzania ni ukurasa mpya kabisa katika maisha yake ya soka, lakini ameanza kuupenda tangu siku za mwanzo.
“Ni uzoefu mpya kabisa kwangu, hii ndiyo mara yangu ya kwanza kufika Afrika, nimecheza katika nchi mbalimbali, lakini nilichokikuta hapa ni watu wenye ukarimu mkubwa, nimekuwa hapa kwa siku chache, bado najifunza mambo mengi lakini hisia za mwanzo ni nzuri sana,” anasema.
KOTOKA VIENNA HADI AFRIKA
Canadi anasema safari yake ya soka ilianzia Austria, alikozaliwa na kujiunga na akademi ya Austria Vienna akiwa mdogo.
Anasema kucheza katika tamaduni tofauti kumemjenga kuwa mchezaji anayeelewa mahitaji ya kila mazingira na sasa anaamini Tanzania ni sehemu nyingine ya safari yake ya mafanikio.
KWA NINI SINGIDA BS?
Wengi walishangaa kuona mchezaji mwenye historia ya kucheza Ulaya akichagua kuja Tanzania, lakini Čanadi anasema hakuhitaji kushawishiwa sana.
Anasema aliona mradi wa Singida Black Stars una malengo makubwa huku ushiriki wa timu hiyo katika michuano ya CAF ukiwa moja ya sababu zilizomvutia.
“Nimefurahi kuwa sehemu ya kikosi hiki. Nataka kuleta ubora wangu, uzoefu wangu na kusaidia timu kufikia mafanikio makubwa msimu huu,”
LENGO NI AFRIKA
Msimu huu Singida Black Stars inakabiliwa na ratiba ngumu ya mashindano matatu makubwa, Canadi anaamini kikosi walichonacho kina uwezo wa kupambana katika kila mashindano huku akisisitiza kuwa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ndiyo malengo yao ya kwanza.
“Najua kutakuwa na mechi nyingi sana. Bado ninajifunza kuhusu ligi na timu mbalimbali, lakini kila mchezo huanza kwa matokeo ya 0-0. Tutapambana kwa nguvu zote. Nataka kufunga mabao, kutoa pasi za mwisho na kusaidia timu kupata matokeo mazuri,” anasema.
KUHUSU SOKA LA AFRIKA
Kuhusu tofauti kati ya soka la Afrika na Ulaya, Čanadi anasema jambo lililomvutia zaidi ni kasi kubwa ya wachezaji wa Afrika.
Kwa mtazamo wake, Ulaya imejikita zaidi kwenye mbinu na umiliki wa mpira, wakati Afrika imebarikiwa kasi, nguvu na uwezo mkubwa wa mchezaji mmoja mmoja.
“Kila nchi ina mfumo wake wa soka, hapa nimeona kasi kubwa sana ya mchezo. Ulaya kuna mbinu nyingi zaidi na umiliki wa mpira. Ukiweza kuunganisha vitu hivyo viwili, utapata timu bora.”
Kabla ya kuwasili nchini, Canadi anasema alizungumza na rafiki yake mmoja na alimuelezea mazingira ya ligi, maisha ya hapa na ushindani uliopo. Mbali na maelezo hayo, pia ametazama video mbalimbali za mechi za Ligi Kuu Bara ili kupata picha ya aina ya soka atakayokutana nalo.
CHAKULA CHA TANZANIA
Pamoja na kuja kwa ajili ya soka, Canadi amesema kuna jambo moja ambalo limemvutia haraka kuliko mengine.
“Kitu cha kwanza kilichonifurahisha ni chakula. Kimekuwa kizuri sana tangu nilipofika,” anasema.
Ingawa bado hajaanza kuonyesha vitu vyake, Canadi amesema anasubiri kwa hamu kukutana na mashabiki.
“Nimejiandaa. Nipo fiti na nataka kushindana uwanjani. Mashabiki wanapaswa kutarajia soka la kuvutia kutoka kwangu. Nataka kufunga mabao mengi, kutoa pasi za mabao na kusherehekea ushindi pamoja nao,” anasema.
KUBWA ZAIDI KATIKA LIGI KUU BARA
Muda utaongea kwa Mzungu huyo wa Bundesliga kama ataweza kuhamisha ubora wake kutoka viwanja vya Ulaya hadi nyasi za Tanzania na kuiongoza Singida Black Stars kutimiza ndoto zake za kutamba Afrika au laa.