Simba, Yanga yasogezwa tena mbele

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetangaza kusogeza mbele muda wa kuchezwa mechi ya Simba dhidi ya Yanga kutoka saa 11:00 jioni hadi saa 1:00 usiku.

Taarifa waliyoitoa mchana huu TFF imeeleza kuwa sababu ya kuahirisha ni maelekezo kutoka Wizara Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Awali mechi hiyo ilibidi kuchezwa Machi 8 na ikasogezwa Mei 8 saa 11:00 jioni na sasa imesogezwa saa 1:00 usiku.

"TFF inawafahamisha wadau kuwa mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Simba SC na Yanga SC iliyokuwa ianze saa 11 jioni sasa itaanza saa 1 usiku. TFF imepokea maelekezo ya mabadiliko ya muda wa kuanza mchezo kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo," imeeleza taarifa hiyo.

Baada ya kupata taarifa hiyo, Mwanaspoti lilianza kuwafuata mashabiki wa timu zote mbili walioonekana kuwa na hasira na kuzungumza nao ambapo wametoa mawazo yao juu ya habari hiyo ya kusogezwa mbele kwa mechi.

“Hii inaonesha namna gani mashabiki wa  soka Tanzania hatuheshimiwi, jana tulitangaziwa kabla ya saa 10 jioni tuwe tayari uwanjani na baada ya hapo hatutaruhusiwa kuingia ndani.

Tumejipanga na familia nzima, tumeingia uwanjani tangu saa 5:00 asubuhi alafu muda huu wanatuambia mechi saa 1:00, hii imeniumiza sana mimi na familia yangu na hivi unavyoona ndio mwisho wangu kuja kutizama mechi kwenye uwanja huu,” alisema Gozi shabiki wa Yanga aliyeambatana na Familia yake.

“Bongo muda mwinginee suala la ‘On Time’huwa ni gumu sana, ukichelewa unaambiwa unazingua, ukiwahi wao wanakuzingua sasa ndio nini hii, hii ni dhahiri kuwa mashabiki wa Bongo hatuthaminiwi,” anasema Getruda, shabiki wa Simba.

Haijaishia hapo, Mwanaspoti liliendelea kuzungumza na mashabiki wa timu hizo mbili huku wengi wakionekana kuzitupia lawama taasisi zinazoongoza michezo hususani Soka hapa nchini.

“Nashindwa hata niseme nini, we unaona hii ni sawa?, yaani muda wote najua mechi ni saa 11:00 jioni alafu hao TFF wanasema ni saa 1:00!, basi watupe chakula maana wengine hatujala tangu asubuhi na tumekwisha ingia ndani na hatuwezi kutoka,” alisema Jidi shabiki wa Simba aliyeonekana kuwa na hasira.

“Hivi hawa TFF wanatuchukuliaje sisi?. Yaani tujipake marangi hivi, tulipe viingilio, tushinde njaa halafu wanatuambia mechi imesogezwa mbele, hii sio haki, tutawaambiaje wame zetu tukirudi tumechelewa huku tuliaga tutarudi mapema, kiukweli wametukosea,” alisema Mama Kamusoko shabiki wa Yanga aliyekuwa amejipaka rangi za kijani na njano usoni mwake.