Simba yamfukuzia staa wa Yanga Princess
Muktasari:
- Kumpata Kalsa kunaweza kuisaidia timu hiyo kutokana na uzoefu alioupata akiwa Yanga Princess, ambako alikuwa miongoni mwa wachezaji waliotegemewa katika eneo la kiungo.
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania, Simba Queens, wameanza kumfuatilia kwa karibu kiungo wa zamani wa Yanga Princess, Aregash Kalsa, wakitaka kumsajili ili kuongeza nguvu katika kikosi chao kinachojiandaa na changamoto za msimu huu.
Kalsa, aliyewahi kuwa miongoni mwa viungo tegemeo wa Yanga Princess, alijiunga na timu hiyo akitokea C.B.E ya Ethiopia na kuitumikia kwa misimu miwili mfululizo kabla ya safari yake ndani ya kikosi hicho cha Jangwani kufikia mwisho msimu uliopita.
Kiungo huyo aliondoka Yanga Princess baada ya mkataba wake kumalizika, huku viongozi wa klabu hiyo wakiamua kutomuongezea mkataba mpya, hali iliyomwacha akiwa huru kutafuta changamoto nyingine.
Sasa baada ya Yanga kuachana naye Simba Queens inatajwa kuwa katika mchakato wa kuhakikisha inamnasa nyota huyo ambaye kwa sasa hana timu, ikiwa ni sehemu ya mipango yake ya kuimarisha kikosi hicho.
Taarifa zinaeleza kuwa Simba Queens tayari imepeleka ofa kwa kiungo huyo, ingawa bado haijafahamika iwapo amekubali pendekezo hilo au kama mazungumzo baina ya pande hizo yanaendelea.
"Ni mchezaji mzuri ambaye Simba wanamuona anaweza kuongeza nguvu kwenye eneo la ushambuliaji, bado hawajamalizana lakini tayari Simba imetuma ofa ikisikilizia hadi dirisha dogo maendeleo yake."
Kumpata Kalsa kunaweza kuisaidia timu hiyo kutokana na uzoefu alioupata akiwa Yanga Princess, ambako alikuwa miongoni mwa wachezaji waliotegemewa katika eneo la kiungo.