Crawford aingia Dunda, kulea vipaji Tanzania
Muktasari:
- Crawford alishiriki uzinduzi wa ligi hiyo pamoja na mchujo wa mabondia wanaowania nafasi za kushiriki mashindano hayo, yanayotarajiwa kuanza baadaye mwaka huu jijini Dar es Salaam.
BINGWA wa zamani wa dunia katika ndondi za kulipwa, Terence “Bud” Crawford, amekubali kuwa mlezi wa Ligi ya Ngumi za Kulipwa Tanzania, Dunda, inayolenga kuibua na kukuza vipaji vya mabondia chipukizi nchini.
Crawford alishiriki uzinduzi wa ligi hiyo pamoja na mchujo wa mabondia wanaowania nafasi za kushiriki mashindano hayo, yanayotarajiwa kuanza baadaye mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Ligi hiyo inaendeshwa kwa ushirikiano wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) na kituo cha redio cha Times FM, ikiwa na lengo la kuimarisha maendeleo ya mchezo huo na kuwapa mabondia wenye vipaji nafasi ya kujijenga na kujulikana ndani na nje ya nchi.
Crawford, bondia wa Marekani aliyejizolea mataji ya dunia katika uzani tofauti na kumaliza rekodi yake ya ndondi za kulipwa bila kupoteza pambano, alishiriki uzinduzi wa Dunda uliofanyika Mei 25, 2026, jijini Dar es Salaam.
Baadaye, Oktoba 3 na 4 mwaka huu, alishiriki pia katika shughuli za mchujo wa mabondia wanaowania nafasi za kuingia kwenye ligi hiyo, ambapo mamia ya washiriki walijitokeza kuonyesha uwezo wao mbele ya majaji wenye uzoefu.
Makamu wa Rais wa TPBRC, Jacob Mbuya, amesema Crawford atakuwa mlezi wa ligi hiyo, ambayo inatarajiwa kuanza rasmi baadaye mwaka huu.
“Kwa nafasi yake kama mlezi na balozi wa kimataifa wa Dunda, Crawford anatarajiwa kusaidia kuhamasisha na kuendeleza vipaji vya mabondia wanaochipukia,” amesema Mbuya.
Ameongeza kuwa maandalizi yamefikia hatua muhimu baada ya kukamilika kwa mchujo wa mabondia watakaoshiriki mashindano hayo.
Kwa mujibu wa Mbuya, majina ya mabondia waliofaulu mchujo yatatangazwa Novemba mwaka huu, sambamba na kutolewa kwa tarehe rasmi ya kuanza kwa ligi, mfumo wa mashindano na ratiba ya mapambano.
“Bondia watakaotangazwa kuwa wamefaulu mchujo watashiriki ligi hii, ambayo lengo lake ni kuwapatia mabondia nchini mapambano ya mara kwa mara ili kuongeza uzoefu, kujenga rekodi zao na kuwaandaa kwa hatua za juu za ndondi za kulipwa kimataifa,” amesema.
Akizungumzia umuhimu wa Crawford katika ligi hiyo, Mbuya amesema wanatarajia uzoefu na rekodi ya bondia huyo vitakuwa chachu kwa washiriki, huku vikiwasaidia kuona fursa zilizopo katika ndondi za kulipwa kimataifa.
Crawford amejenga jina kubwa katika mchezo huo kutokana na mafanikio yake katika uzani tofauti. Rekodi yake ya kutopoteza pambano lolote katika ndondi za kulipwa imemweka miongoni mwa mabondia waliovutia hisia za mashabiki duniani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kuhusu historia yake, pambano lake dhidi ya Saul “Canelo” Alvarez la Septemba 13, 2025, lilimalizika kwa ushindi wa Crawford kwa pointi baada ya raundi 12. Hadi kufikia hatua hiyo, alikuwa ameshinda mapambano yote 42 aliyocheza, yakiwamo 31 kwa KO.
Tangu alipoanza ndondi za kulipwa Machi 2008, Crawford ametwaa mikanda mbalimbali ya dunia katika uzani tofauti na kuweka historia katika mchezo huo.
Miongoni mwa mabondia wakubwa aliowahi kuwashinda ni Alvarez, Errol Spence Jr, Amir Khan, Shawn Porter na Kell Brook.
Ujio wake katika Dunda unatarajiwa kuongeza mvuto wa ligi hiyo, huku wadau wa ndondi nchini wakilenga kutumia mashindano hayo kujenga kizazi kipya cha mabondia wenye uwezo wa kushindana katika medani za kimataifa.