Alliance Girls yakomaa sehemu za ulinzi
Muktasari:
- Alizitaja timu za Bilo Queens na Iboma Queens ni miongoni mwa wapinzani waliocheza nao katika maandalizi hayo na wamepata nafasi ya kucheza dhidi ya vijana kwa lengo la kuwajenga wachezaji na kuboresha kiwango chao.
KOCHA wa Alliance Girls, Sultan Juma amesema timu hiyo inaendelea kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika mechi za kirafiki na eneo la ulinzi ni miongoni mwa sehemu zinazohitaji maboresho kabla ya kurejea kwa Ligi Kuu ya Wanawake.
Juma amesema wamekuwa wakitumia mechi za kirafiki kupima uwezo wa wachezaji na kubaini maeneo ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi ili kuhakikisha kikosi kinakuwa katika kiwango bora zaidi ligi itakaporejea.
Alizitaja timu za Bilo Queens na Iboma Queens ni miongoni mwa wapinzani waliocheza nao katika maandalizi hayo na wamepata nafasi ya kucheza dhidi ya vijana kwa lengo la kuwajenga wachezaji na kuboresha kiwango chao.
"Tumecheza mechi tatu za kirafiki, ikiwemo dhidi ya Bilo Queens, Iboma Queens na tumewaelekeza vijana namna gani ligi ilivyo ngumu. Tunatumia michezo hiyo kuona maeneo ambayo tunahitaji kuyafanyia kazi," amesema Juma.
Ameongeza eneo la ulinzi bado lina changamoto ambazo benchi la ufundi linaendelea kuzifanyia kazi, akisisitiza lengo lao ni kuhakikisha timu inakuwa imara zaidi na kupunguza makosa yanayoweza kuigharimu wanapokuwa kwenye ushindani wa ligi.
Kocha huyo amesema pamoja na mapungufu yaliyopo, ana matumaini maandalizi wanayoendelea kuyafanya yatazaa matunda na kuifanya Alliance Girls irejee ikiwa bora zaidi.
Alieleza wanaendelea kuwapa wachezaji maelekezo na kufanya marekebisho kulingana na kile wanachokiona katika michezo ya kirafiki wanayoendelea kucheza.
Hata hivyo, Juma amesema bado hawajapata taarifa rasmi kuhusu tarehe ya kuanza tena kwa ligi hiyo, licha ya awali kuambiwa kuwa ingeanza Oktoba 23.