Prime
Simba yahaha na straika dakika za mwisho
WAKATI dirisha la usajili likifungwa jana saa 5:59 usiku, mabosi wa Simba walikuwa bize kupambana na JKT Tanzania ili kuipata saini ya mshambuliaji hatari wa kikosi hicho, Paul Peter Kasunda.
Taarifa kutoka ndani ya Simba zimeliambia Mwanaspoti mshambuliaji huyo aalikuwa anapigiwa hesabu kwenda kuongezea nguvu eneo la ushambuliaji ili liwe hatari zaidi, licha ya kukamilisha pia usajili wa mshambuliaji wa Mashujaa, Ismail Mgunda.
Hatua ya Simba kuanza msako huo ni baada ya kupata pigo la kuondokewa na mshambuliaji, Seleman Mwalimu ‘Gomez’, ambaye amejiunga na watani zao wa jadi Yanga kwa mkopo akitokea Wydad Casablanca ya Morocco, licha ya matarajio makubwa kwake.
Mwalimu aliyecheza Simba kwa mkopo msimu wa 2025-2026 na kufunga mabao tisa ya Ligi Kuu Bara akitokea Wydad Casablanca, alikuwa katika hatua za mwisho za kujiunga na kikosi hicho tena, japo, Yanga ilipindua dili hilo na kuipata saini yake.
Akizungumza na Mwanaspoti, meneja wa mchezaji huyo, Rashid Malambi ‘Ugege’ alisema ni kweli Simba imeulizia upatikanaji wa Paul Peter na kuwataka ianze kwanza kuzungumza na waajiri wake JKT Tanzania, kabla ya uongozi wao kufanya uamuzi huo.
“Tangu msimu uliopita tulipata ofa mbalimbali kutoka klabu za ndani na nje ya nchi, lakini hazikuweza kufikia maslahi tuliyoyahitaji, mazungumzo hayo yameendelea pia hadi sasa, ingawa hakuna muafaka rasmi tuliokubaliana nafikiri hadi usiku walikuwa wanahaha, ngoja tuone watafikia wapi,” alisema Malambi.
Peter aliyeanzia timu ya vijana ya Azam chini ya miaka 20 kabla ya kupandishwa kuchezea ya wakubwa amekuwa ni mhimili mkubwa kwa kikosi hicho cha maafande msimu huu, kutokana na kiwango bora anachoendelea kukionyesha hadi sasa.
Mshambuliaji huyo aliyepandishwa kuichezea Azam na aliyekuwa kocha wa kikosi hicho Mromania Aristica Cioaba, amechezea pia timu mbalimbali zikiwemo za Mugabe, KMC, maafande wa Tanzania Prisons, Dodoma Jiji, kisha kutua JKT Tanzania.