Mashujaa ilivyofunga milango ya usajili
Muktasari:
- Uamuzi huo umefikiwa baada ya uongozi wa Mashujaa kuamini kuwa kikosi kilichopo kina idadi na ubora wa kutosha katika eneo la ushambuliaji, hasa baada ya kusajili wachezaji wapya ambao wanatarajiwa kuongeza nguvu katika safu hiyo msimu ujao.
MASHUJAA FC imefunga milango ya usajili katika eneo la ushambuliaji, ikisisitiza kuwa haina mpango wa kuongeza mchezaji mwingine katika nafasi hiyo hata kama mshambuliaji Ismail Mgunda atamalizana na Simba.
Uamuzi huo umefikiwa baada ya uongozi wa Mashujaa kuamini kuwa kikosi kilichopo kina idadi na ubora wa kutosha katika eneo la ushambuliaji, hasa baada ya kusajili wachezaji wapya ambao wanatarajiwa kuongeza nguvu katika safu hiyo msimu ujao.
Hivyo, licha ya uwezekano wa mabadiliko katika benchi la ufundi endapo Mgunda atakamilisha dili lake kabla dirisha halijafungwa leo usiku, taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zilieleza kuwa suala hilo halitabadilisha mipango ya usajili katika eneo la ushambuliaji.
“Kocha ameshatuambia hata kama Mgunda ataondoka basi hatuna haja ya kufanya usajili tena kwani hakuna nafasi zinazohitajika na sasa kazi kubwa ni kwa benchi la ufundi kuwatengeneza wachezaji wapya kuwa sehemu ya mfumo wa timu.”
Miongoni mwa washambuliaji wapya waliosajiliwa na Mashujaa ni Michael Joseph, mshambuliaji aliyekuwa mfungaji bora wa KVZ ya Zanzibar, ambaye anatarajiwa kuwa moja ya silaha muhimu katika kikosi hicho.
Mbali na Joseph, Mashujaa imemsajili Omari Mponda kutoka Mbuni FC, huku pia ikiongeza nguvu kwa kuwasajili Mishamo Daud na Machela Julius, wote wakiwa katika eneo la ushambuliaji.
Rekodi ya msimu uliopita inaonyesha Mashujaa ilikuwa na washambuliaji kadhaa waliopata nafasi ya kucheza, lakini idadi ya mabao ilikuwa bado haijafikia kiwango ambacho kingeifanya timu hiyo kuwa miongoni mwa timu zenye safu kali zaidi za ushambuliaji.
Ukianza kwa Mgunda ambaye alicheza mechi 10 na kufunga bao moja pekee, Crispin Mhagama akiwa amecheza mechi 23 na kufunga mabao matatu, wakati Seif Rashid Abdallah alicheza mechi 16 na kufunga mabao matatu.
Hussein Juma Mihambo alicheza mechi 10 na kufunga bao moja, huku Daniel Lyanga akicheza mechi 10 bila kufunga bao. Emmanuel Martin, kwa upande wake, alipata mechi saba bila kufunga.
Winga David Ulomi alikuwa miongoni mwa waliokuwa na mchango mkubwa zaidi, akicheza mechi 23 na kufunga mabao matano.
Takwimu hizo zinaonyesha kuwa washambuliaji waliokuwepo msimu uliopita hawakuwa na uzalishaji mkubwa wa mabao, jambo ambalo linaeleza kwa kiasi kikubwa sababu ya klabu kuamua kuleta sura mpya nyingi katika eneo hilo.