Simba yagawa barua kwa mastaa, yavamia ASEC kufuata winga

Muktasari:

  • Winga ambaye Simba ipo naye kwenye mazungumzo mazito kuhakikisha inaipata saini yake kuja kuongeza nguvu zaidi kikosini anatajwa kwa jina la Kramo Aubin.

SIMBA ipo sokoni kuangalia silaha za kuondoa aibu kwa msimu ujao na unyonge wa mashabiki wanaoupitia kwa msimu huu, ikidondosha mataji yote, tayari imetua nchini Ivory Coast ikiwinda winga la ASEC Mimoses, huku mastaa wakilimwa barua.

Winga ambaye Simba ipo naye kwenye mazungumzo mazito kuhakikisha inaipata saini yake kuja kuongeza nguvu zaidi kikosini anatajwa kwa jina la Kramo Aubin.
Huyo jamaa ni hatari kwa mikimbio na Simba ilishaonja joto la jiwe la mchezaji huyo aliwahi kuwafunga mwaka 2022 walipocheza Kombe la Shirikisho la Afrika, wakichapwa mabao 3-0 ugenini lakini pia msimu huu amekuwa bora kwenye michezo yote.

Wakati winga huyo akitajwa kuna asilimia kubwa ya kujiunga na Wanamsimbazi, dili hilo likitiki atapishana na Augustine Okra, Nelson Okwa, Ismael Sawadogo na Gadiel Michael ambao tayari wamepewa barua za kwaheri klabuni hapo.

Mastaa hao tayari wamepewa barua za kuachana na timu hiyo baada ya kushindwa kuonyesha uwezo ambao walikuwa wanautarajia kutoka kwao Okrah, Okwa walisajiliwa dirisha kubwa la usajili msimu huu wakati Sawadogo akisajiliwa dirisha dogo huku Gadiel alijiunga na Simba akitokea Yanga msimu wa 2019.

Kati ya mastaa hao waliopewa mkono wa kwaheri Mwanaspoti lilifanikiwa kumpata Gadiel Michael ambaye alisema ni kweli mkataba wake unamalizika msimu huu lakini bado hajafahamu hatima yake.

"Ishu ya barua? nakusikia wewe na kuhusu mazungumzo ya mkataba mpya au kwenda timu nyingine bado sijafanya uamuzi wowote hadi sasa nasubiri msimu umalizike, bado kuna michezo miwili mbele natakiwa kucheza na mimi ni mchezaji wa Simba." alisema beki huyo.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kililiambaia Mwanaspoti kuwa uongozi upo kwenye hatua nzuri za mazungumzo kwa ajili ya kumalizana na staa huyo wa Asec ambaye wanaamini ataweza kuongeza kitu ndani ya timu.

"Tumeondoa wachezaji wawili ambao wanacheza nafasi ya winga na kocha amependekeza kusajiliwa kwa wachezaji wawili kwenye nafasi hiyo mgeni mmoja na mzawa mmoja ambaye anaweza kucheza miguu yote miwili;

"Mazungumzo na winga huyo ambaye ni mchezaji tegemeo wa kikosi cha ASEC Mimosas yanakwenda vizuri na kuhusu mchezaji mzawa tumemwambia kocha amfuatilie Shiza Kichuya kwasababu ni winga ambaye anasifa kama alizozitaja, hivyo tunamsikilizia kama mambo yatakwenda kama ilivyopangwa tutaweza kufanya naye mazungumzo." kilisema chanzo hicho ambacho hakikutaka jina lake litajwe kwenye gazeti.

Chanzo hicho kililiambia Mwanaspoti kuwa wanaendelea na usajili ili kukiandaa kikosi chao mapema kama mapendekezo ya kocha wao alivyotaka kuona wanasajili mapema ili kuingia kambini mapema kujiandaa na msimu mpya.
Kramo Aubin amecheza mechi nane za Kombe la Shirikisho Afrika na kuifungia timu yake mabao manne kwenye michezo hiyo moja alilifunga uwanja wa nyumbani na matatu kwenye michezo ya ugenini.

Staa huyo amecheza timu tatu tu hadi sasa zote zikiwa za nchini kwao Ivory Coast amekuzwa na ASEC Mimosas ambayo alianza kuitumikia mwaka 2015 akicheza kwa misimu miwili baadae akatimkia Africa Sports alicheza msimu mmoja, 2019 alitimkia FC San Penro na 2021 akaamua kurudi tena ASEC Mimosas ambayo anaitumikia hadi sasa.