Prime
Simba yacheza akili kubwa kwa straika mpya
MABOSI wa Simba wanaendelea kufuatilia maendeleo ya mshambuliaji wa JKT Tanzania, Paul Peter Kasunda baada ya kumkosa katika dirisha la usajili lililofungwa Agosti 15, 2026, kutokana na kutofikia makubaliano na waajiri wake.
Simba ilikuwa inahaha kupata saini ya mshambuliaji huyo ili kwenda kuongeza makali ya safu ya ushambuliaji, inayoongozwa na Ibrahim Doumbia ambaye bado hajaonyesha makali yake na Ismail Mgunda aliyesajiliwa akitokea Mashujaa.
Taarifa kutoka Simba, zimeliambia Mwanaspoti kwamba, mshambuliaji huyo anapigiwa hesabu za kujiunga na timu hiyo katika dirisha dogo la Januari 2027, ikiwa Doumbia na Mgunda watashindwa kuendana na kasi ya kikosi hicho cha Kocha Mkuu, Steve Barker.
“Baada ya kumkosa dirisha kubwa, bado hatujakata tamaa ya kufuatilia maendeleo yake, tuna imani kubwa na washambuliaji waliopo, ila ikiwa watashindwa kuendana na kasi tunayoitaka kwa sasa tutamsajili ili atusaidie,” kilisema chanzo hicho.
Akizungumza na Mwanaspoti, meneja wa mchezaji huyo, Rashid Malambi ‘Ugege’ alisema baada ya uongozi wa Simba kumuulizia mchezaji huyo waliwaelekeza wazungumze kwanza na waajiri wake JKT Tanzania, lakini walishindwa kutimiza kile walichoambiwa.
“Sisi tunaheshimu uhusiano wetu na JKT Tanzania, timu inayotaka mchezaji yeyote ni lazima kwanza izungumze nao ili iwe urahisi kwa pande mbili, ikiwa watakuja mezani tutakaa chini na kuangalia ofa iliyokuwa bora zaidi,” alisema Malambi.
Paul Peter aliyewahi kuanzia timu ya vijana ya Azam chini ya miaka 20, hadi kupandishwa kuchezea ya wakubwa, amekuwa ni muhimili mkubwa kwa kikosi hicho cha maafande msimu huu, kutokana na kiwango bora anachoendelea kukionyesha hadi sasa.
Mshambuliaji huyo aliyepandishwa kuichezea Azam na aliyekuwa kocha wa kikosi hicho, Mromania Aristica Cioaba, amechezea pia timu mbalimbali zikiwemo za Mugabe FC, KMC, Tanzania Prisons, Dodoma Jiji, kisha JKT Tanzania.
Nyota huyo alijiunga na JKT, Julai 9, 2025, akitokea Dodoma Jiji, baada ya msimu wa 2024-2025, kufunga mabao manane ya Ligi Kuu, akiwa nafasi ya pili kwa wachezaji wazawa waliofunga mabao mengi, nyuma ya Clement Mzize wa Yanga aliyefunga 14.
Msimu wa 2025-2026, akiwa na JKT, aliifungia mabao tisa ya Ligi Kuu na matano ya Kombe la CRDB na mbali na Simba ambayo imeonyesha nia ya kumuhitaji, ila ZED FC ya Misri na Al-Dahra Tripoli FC ya Libya ni miongoni mwa timu zinazomuhitaji.