Simba mwendo wa shoo tu, Sakho aibua vita mpya
SIMBA imekubali yaishe kwa kushindwa kutwaa ubingwa wa michuano yoyote kwa msimu huu, baada ya juzi Yanga kutwaa taji la Ligi Kuu Bara, baada ya awali kunyakua Ngao ya Jamii ikiizima Wekundu hao kwa mabao 2-1, lakini kocha wa timu hiyo amewahakikishia shoo tamu hadi mwisho.
Simba imesaliwa na mechi mbili za kufungia msimu ikiwa tayari pia imeshatolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC) ikifungwa na Azam mabao 2-0 katika mechi ya nusu fainali, huku ilikosa pia Kombe la Mapinduzi 2023, mechi zote zikipigwa jijini Dar es Salaam.
Timu hiyo yenmye mataji 22 ya Ligi Kuu Bara, saba pungufu na iliyonayo Yanga yenye 29, itavaana na Polisi Tanzania kisha kumalizana na Coastal Union, ambapo ikishinda zote itafikisha pointi 73 ambazo zimeshapitwa na Yanga yenye 74 na michezo miwili mkononi.
Licha ya kutambua kuwa haina chake, Kocha Roberto Oliveira 'Robertinho' aliliambia Mwanaspoti kwamba, ameshaufunga msimu lakini bado anataka timu yake iendelee kuwapa raha mashabiki wakati ikijiandaa kwa msimu ujao itakapojipanga kivingine.
Robertinho alisema amezungumza na wachezaji ili wacheze soka tamu zaidi na kupata matokeo mazuri kwenye mechi zilizosalia ili wasiwatie unyonge mashabiki ambao wamekosa furaha kwa kuona timu hiyo ikishindwa kuambulia taji lolote tofauti na malengo yaliyokuwa yamewekwa hapo awali.
"Ligi imeisha kwa upande wa ubingwa, lakini mechi bado zipo na mashabiki wanastahili kupata raha kwa kuendelea kupata matokeo mazuri, nimezungumza na wachezaji na hata mliona tulivyocheza na Ruvu Shooting, tunataka kupambana kumaliza kwa heshima, hata kama hatuna taji," alisema kocha huyo kutoka Brazili aliyeajiriwa mwanzoni mwa mwaka huu kuchukua nafasi ya Zoran Maki.
Robertinho alisema wanasimba hawana wa kumlaumu kwani soka ndivyo lilivyo, iwapo hasa ugumu uliokuwapo tangu mwanzo wa msimu hata kabla ya kuja nchini na wakati akiinoa na kupambana kadri ya uwezo wao ili kutimiza malengo, lakini mambo yakaenda vibaya ndani na kimataifa.
Licha ya kukosa mataji, Simba imevunja rekodi ilizokuwa nazo kwa msimu uliopita ilipozidiwa ujanja pia na Yanga na kuporwa ubingwa iliyokuwa ikishikilia kwa misimu minne mfululizo, kuanzia idadi ya pointi ilizonaliza nazo hadi mabao ya kufunga na kufungwa.
Msimu uliopita Simba ilimaliza nafasi ya pilio nyuma ya Yanga ikiwa na pointi 61, ambazo zimeshazipita msimu huu hadi sasa kwani ina pointi 67 huku ikiwa na michezo miwili mkononi inayoweza kuziongeza, puia ilifunga mabao 41 wakati msimu huu ina 66 hadi sasa.
Pia msimu uliopita ilishinda jumla ya mechi 17 kati ya 30, wakati msimu huu imeshinda 20, huku ikitoka sare saba, tofauti na msimu uliopita ilipata sare 10 na kupoteza mechi tatu, wakati msimu huu hadi sasa imepoteza mchezo mmoja tu iliypofungwa na Azam FC.
Kwa mabao ya kufungwa msimu uliopita iliruhusu machache zaidi yakiwa 14, ila msimu huu tayari hadi sasa imefungwa 15.
SAKHO AIBUA VITA MPYA
Katika hatua hatua nyingine kiungo mshambuliaji machachari wa timu hiyo, Pape Ousmane Sakho ameibua vita mpya baada ya wikiendi iliyopita kufunga mabao mawili na kubanana na nahodha wake, John Bocco kila mmoja akiwa na mabao tisa.
Sakho ambaye amekuwa hana nafasi katika kikosi cha kwanza, ameibuka mwishoni kama ilivyokuwa msimu uliopita aliomaliza na mabao sita, ameanzisha vita ya ufungaji mabao ndani ya Simba, lakini akiwa na kibarua cha mechi zilizosalia kuona kama anaweza kumpiku kinara Fiston Mayele wa Yanga mwenye mabao 16 hadi sasa.
Sakho amesaliwa na bao moja tu kwa sasa kumfikia kinara wa mabao wa timu hiyo, Moses Phiri mwenye 10, huku Saido Ntibazonkiza naye akiwa na idadi kama hiyo japo manne alitoka nayo Geita Gold akiwa sambamba na Phiri nyuma ya Mayale.
Kama Sakho ataendelea kupewa nafasi ya kufunga mabao mengi zaidi ana nafasi ya kupiku Phiri na kumaliza kama kinara wa mabao wa klabu hiyo, kwani Mzambia huyo kwa sasa hapewi nafasi na kocha Robertinho.
Ila mambo yakienda hovyo, huenda Simba ikajikuta kwa msimu wa pili mfululizo ikishindwa kutwaa tuzo ya Mfungaji Bora, kwani msimu uliopita ilibebwa na George Mpole aliyekuwa Geita Gold akifunga 7, akimzidi Mayele aliyemaliza na 16 kama aliyonayo kwa sasa ligi ikielekea ukingoni.