Al Hilal yajipoza nafasi ya tatu Kagame
Muktasari:
- Ushindi huo umeifanya Al Hilal kujipoza baada ya kushindwa kufuzu fainali mbele ya Gor Mahia huku ikiondoka na zawadi ya Dola 10,000 (zaidi ya Sh26 milioni ) kwa kumaliza katika nafasi ya tatu.
MIAMBA ya soka ya Sudan, Al Hilal imehitimisha safari yake ya Kombe la CECAFA Kagame 2026 kwa kushinda nafasi ya tatu baada ya kuichapa Jamus SC ya Sudan Kusini mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa mapema leo, Ijumaa kwenye Uwanja wa Amahoro, Kigali.
Ushindi huo umeifanya Al Hilal kujipoza baada ya kushindwa kufuzu fainali mbele ya Gor Mahia huku ikiondoka na zawadi ya Dola 10,000 (zaidi ya Sh26 milioni ) kwa kumaliza katika nafasi ya tatu.
Msimu uliopita, Al Hilal ilifika hatua ya fainali lakini ilishindwa kutwaa ubingwa baada ya kufungwa mabao 2-1 na Singida Black Stars kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, hivyo safari ya mwaka huu imeishia hatua moja nyuma.
Mchezo huo ulianza kwa kasi huku timu zote zikicheza kwa tahadhari na kushambuliana kwa zamu katika kipindi cha kwanza. Licha ya kutengeneza nafasi kadhaa, hakuna upande uliotikisa nyavu katika dakika 45 za kwanza.
Al Hilal ilivunja ukimya dakika ya 54 kupitia kwa mshambuliaji wake Ansumana Samura, aliyefunga bao lake la tatu katika michuano hiyo.
Dakika nne baadaye, Jamus ilipata nafasi nzuri ya kurejea mchezoni lakini Laurent Ramazani alishindwa kutumia vyema mkwaju wa penalti waliopata.
Al Hilal iliendelea kutawala mchezo na juhudi zake zilizaa matunda dakika ya 66, Abdelrazig Omer alipopachika bao la pili kwa shuti lililomshinda kipa wa Jamus na kuongeza ugumu kwa wapinzani wao.
Katika dakika za jioni (90+2), Jamus ilipata bao la kufutia machozi kupitia kwa Simon lakini halikutosha kuizuia Al Hilal kuondoka na ushindi katika mchezo huo.
Kwa ushindi huo, Al Hilal imemaliza katika nafasi ya tatu huku macho na masikio sasa yakielekezwa kwenye mchezo wa fainali utakaowakutanisha wenyeji Rayon Sports ya Rwanda na Gor Mahia ya Kenya.
Bingwa wa Kombe la CECAFA Kagame mwaka huu ataondoka na kitita cha Dola 30,000 huku mshindi wa pili akijinyakulia Dola 20,000.