Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Siku 52 Yanga kuweka rekodi

Muktasari:

  • Kati ya mataji hayo tayari imetwaa moja la Ngao ya Jamii ya kufungua msimu wa Ligi Kuu Bara ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba na sasa inavizia taji la Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho Afrika na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Dar es Salaam. Yanga ina siku 52 za kuandika historia kuwa timu ya kwanza Tanzania kutwaa mataji manne ndani ya msimu mmoja ikiwa itachanga vyema karata katika mashindano matatu tofauti inayoshiriki.

Kati ya mataji hayo tayari imetwaa moja la Ngao ya Jamii ya kufungua msimu wa Ligi Kuu Bara ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba na sasa inavizia taji la Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho Afrika na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Katika siku 52, Yanga inakabiliwa na mechi tano za Ligi Kuu Bara ambapo kati ya hizo ikipata ushindi katika mechi mbili itatwaa ubingwa na baada ya hapo itakuwa na mchezo wa nusu fainali ya ASFC dhidi ya Singida Big Stars ambao kama itaibuka na ushindi itatinga fainali ambayo imepangwa kuchezwa Juni 3.

Kibarua kigumu zaidi kwa Yanga ni kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika ambalo kwa sasa ipo katika hatua ya robo fainali ambayo imepangwa kukutana na Rivers United ya Nigeria.

Kama Yanga ikipenya dhidi ya Rivers United itakutana na mshindi kati ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini na Pyramids FC katika nusu fainali ili kuisaka hatua ya fainali ambayo Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika limepanga mechi zake mbili kuchezwa mwishoni mwa Mei na mwanzoni mwa Juni.

Mchezo wa kwanza wa hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika utachezwa Mei 28 na wa marudiano na wa mwisho umepangwa kuchezwa Juni 3.

Kwa sasa, Yanga na Simba ndizo timu ambazo zimewahi kutwaa idadi kubwa ya mataji ndani ya msimu mmoja ambapo kila moja iliwahi kuchukua mataji matatu - yote yakiwa ni ya mashindano ya ndani.

Katika msimu wa 2015/2016, Yanga ilitwaa Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Azam na Simba ikafanya hivyo mara mbili ambazo ni msimu wa 2019/2020 na 2020/2021.

Akizungumzia hilo, Kocha msaidizi wa Yanga, Cedrick Kaze alisema ratiba iliyo mbele ni ngumu lakini watapambana kuhakikisha wanaweka historia ya kutwaa mataji hayo.

“Malengo yetu ni kufanya vizuri katika mashindano ya ndani na yale ya Afrika na kote hadi sasa tunaonyesha mwenendo mzuri. Ratiba ni ngumu na tunalazimika kucheza mechi nyingi ndani ya muda mfupi, lakini tutajitahidi kukabiliana nayo ili tuweze kufanya vizuri,” alisema Kaze.

Nyota wa zamani wa Yanga, Abeid Mziba ‘Tekelo’ alisema kuwa uwezekano wa Yanga kutwaa mataji hayo upo ikiwa benchi la ufundi, wachezaji na viongozi watajipanga vilivyo. “Sio jambo rahisi lakini linawezekana ikiwa kila mmoja atatimiza vizuri majukumu yake. Mpira wa sasa umebadilika na Yanga ina kikosi kizuri ambacho kikiandaliwa vizuri tunaweza kuandika historia. Soka letu limekua na hatuna hofu ya kupambana na hizo timu zinazoonekana kubwa,” alisema Mziba.