Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sikia yaliyomkuta yule Busungu wa Yanga

Muktasari:

MAISHA ni kama gwaride, ndio msemo pekee ambao utakuwa sahihi kuutamka pale utakapokutana na Malimi Busungu, straika wa zamani wa klabu za Yanga, Lipuli, Mgambo JKT, Polisi Moro, Coastal Union, Kagera Sugar na Villa Squad.

MAISHA ni kama gwaride, ndio msemo pekee ambao utakuwa sahihi kuutamka pale utakapokutana na Malimi Busungu, straika wa zamani wa klabu za Yanga, Lipuli, Mgambo JKT, Polisi Moro, Coastal Union, Kagera Sugar na Villa Squad.

Maisha kwa upande wake kwa sasa yamebadilika kabisa, sio Busungu yule aliyezitikisa Simba na Yanga wakati anataka kusajiliwa kutokea Mgambo Shooting.

Maisha ya mpira yamempa somo ambalo hatakaa alisahau. Mwanaspoti limebahatika kupiga naye stori na amefunguka mengi kuhusu maisha yalivyokuwa wakati anasakata kabumbu hadi kufikia sasa.

ALITOKAJE YANGA?

“Mkataba wangu uliisha na hakukuwa na mazungumzo ya kutaka kuniongeza mkataba mpya, hivyo ikanibidi niondoke klabuni hapo na kujiunga na Lipuli ya Iringa kwa kuwa mpira ndio kazi yangu,” anasema

“Msimu wa kwanza nikiwa Lipuli ulikuwa mzuri sana, lakini mambo yalikuja kubadilika kwenye msimu wangu wa pili baada ya kuondoka kwa aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Ramadhani Maano kwa sababu kipindi Maano alikuwapo ni mtu aliyesikiliza sana wachezaji linapokuja suala la masilahi yao,” anasema.

“Kuna nyakati alikuwa radhi kutoa hadi kilicho mfukoni mwake ili akupe stahiki yako, lakini baada ya kuondoka mambo yalikuwa tofauti kabisa. Ilikuwa unakaa miezi mitatu bila ya kupata mshahara wako na wakati huo unategemea mpira ili kuendesha maisha yako.

“Kuna baadhi ya timu ndogo hapa Ligi Kuu wachezaji wanapitia nyakati ngumu, sema hawasemi tu, wanabaki kuongea chinichini na wengine majina yao ninayo na tunajuana maisha yetu huku Uswahilini.

“Hivyo mimi baada ya msimu huo wa pili kuingia nilikumbana na shida hiyo ya kutopewa stahiki zangu na nilipokuwa nawafuata viongozi walikuwa hawatoi kauli inayoeleweka na kama unavyojua binaadamu tunatofautiana.”

Anasema: “Binafsi nisingeweza kukaa kimya nikiona nakosa haki yangu, mwisho nikaona kwamba hapo hakuna cha maana ninachofanya, nikaamua kuachana rasmi na mpira, lakini kama yule mwenyekiti angekuwepo Lipuli, basi hadi muda huu ningekuwa nacheza mpira kwa sababu alikuwa ni mtu mzuri.

“Malipo ndio kitu kilichonifanya nikate tamaa kabisa na kuamua kuachana na mpira, kwa sababu niliona kuwa jambo la masilahi linakuwa ni gumu kutimizwa na baadhi ya klabu zetu za Ligi Kuu, hivyo nikaona bora nifanye shughuli nyingine yenye masilahi”.

ANAFANYA NINI SASA?

Mchezaji huyo kwa sasa yupo mkoani Dodoma, lakini anasema,

“naishi (Dodoma), nipo na mama matoto wangu na shughuli kubwa ninayofanya ni kilimo, nimejikita kwenye kilimo ambapo nalima vitunguu na matikiti maji, mashamba yangu yapo kule Bariadi, lakini hizi mvua zimeharibu vitunguu na kunitia hasara kidogo.”

YIKPE ANAMTAMANISHA

Ikiwa ni kazi anayoipenda na daima ataipenda, Busungu anasema soka lingali moyoni kinoma. “Nimekaa nimefikiria, kuna mchezaji mmoja ananitia hasira sana na ananifanya nitake kurudi uwanjani, anaitwa Yikpe, yaani huyu mchezaji sijamuelewa kabisa, nikiangalia kiwango chake ni cha kawaida sana, sielewi alisajiliwaje, yaani yule hata sasa nikirudi namzidi.”

Mastraika gani anawakubali?

“Swali gumu kidogo hilo, lakini kwa wachezaji wa Kitanzania namkubali zaidi Jafary Kibaya wa Mtibwa Sugar, halafu kwa wanaotoka nje namkubali sana Meddie Kagere, tena huyu hata mtoto mdogo ukimuuliza atakwambia shughuli yake.

“Dah! Kuna beki mmoja alikuwa hatari sana, nakumbuka alikuwa anachezea Ruvu Shooting, sidhani kama hadi sasa anacheza mpira anaitwa George Michael Osei, nakumbuka wakati nachezea Coastal Union aliwahi kumvunja mtu mbele yangu, jamaa nilikuwa namuhofia sana.”

Busungu anasema: “Wakati nacheza pale Yanga ile ilikuwa ya moto, siwezi kusema ni mchezaji gani maana wote walikuwa ni wazuri balaa, ilikuwa kupata namba lazima ujipange vilivyo, hivyo nafikiri siwezi kusema kwamba ni mchezaji fulani, wote walikuwa ni shubiri kwangu.”

Anakumbuka matukio gani Yanga, Busungu anasema: “Nayakumbuka matukio kama mawili hivi, la kwanza ni wakati nacheza Yanga, nakumbuka ilikuwa katika moja ya mechi za kimataifa dhidi ya timu kutoka Angola, jina silikumbuki niligongana na mlinda mlango wao na nikavunjika mbavu tatu, la pili ni wakati nacheza Mgambo Shooting niligongana na kiungo wa timu pinzani na nikazimia papo hapo, nilipokuja kuzindika nikajikuta nipo chumbani. L:akini vipi atarudi uwanjani?

“Nipo tayari kurudi tena kwa sasa najifua.”