Hersi: Msimu uliopita tuliteseka, msimu huu raha zitarudi
Rais wa Yanga, Hersi Said, amekiri kuwa licha ya timu hiyo kutwaa baadhi ya mataji msimu uliopita, haikuwa katika kiwango kilichozoeleka, akisema walipitia kipindi kigumu kilichowafanya wao na mashabiki kuteseka.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya msimu mpya, Hersi alisema changamoto kubwa zilizoikumba Yanga zilikuwa usajili ambao haukutoa matokeo yaliyotarajiwa pamoja na majeraha ya mara kwa mara yaliyowakumba wachezaji muhimu.
"Kulikuwa na wakati nilifika hatua sipendi hata kuangalia mechi za timu yangu. Naamini hata ninyi mashabiki mlipitia hisia hizo hizo," alisema Hersi.
Ameongeza kuwa Yanga haikuwa na ubora ilioonyesha katika misimu iliyopita, jambo lililoifanya ishindwe kucheza kwa kiwango walichokizoea.
"Hatukuwa bora kama tulivyokuwa nyuma. Kulikuwa na changamoto nyingi zilizotufanya tushindwe kushindana kwa kiwango na afya ya ushindani ambayo tumeizoea," alisema.
Hersi alisema uongozi umejifunza kutokana na makosa ya msimu uliopita na umeamua kufanya maboresho makubwa ya kikosi ili kuhakikisha hali hiyo haijirudii.
"Tumefanya usajili mkubwa kwa sababu hatutaki kurudia makosa yale. Ilifika wakati tulikuwa tunaomba mechi ziishe haraka, na nikiri kabisa hayo si maisha tuliyoyazoea Yanga," alisema.
Amebainisha kuwa klabu bado haijamaliza shughuli za usajili, huku lengo likiwa ni kujenga kikosi imara kitakachorejesha furaha kwa mashabiki na ushindani wa kweli katika mashindano yote ya msimu ujao.
"Bado hatujamaliza kusajili. Tunataka kuwa na kikosi kitakachowapa mashabiki raha waliyoizoea. Zamani mechi ilipokuwa inamalizika tulikuwa tunakasirika kwa sababu tulitaka kuendelea kucheza. Tunataka kurejea kwenye kiwango hicho tena," alisema Hersi.