Si mchezo, kwa makipa hawa Azam, kina Mayele, Phiri kazi wanayo
KAMBI ya Azam FC mjini El Gouna, Misri ipo katika siku ya nne leo Jumanne, huku mambo yakizidi kunoga kidogokidogo, ambapo kila kocha amekwishaanza kuwanoa watu wake.
Azam FC ina makocha na watalaamu kibao wanaowafua wachezaji, lengo ni kuja kivingine msimu ujao. Tizi wanalopigishwa makipa mjini hapa si mchezo na washambuliaji hatari wa timu tofauti Ligi Kuu Bara akiwemo Fiston Mayele wa Yanga na George Mpole wa Geita Gold kazi watakuwa nayo kukabiliana na makipa hao.
Baada ya kukuletea matukio ya safari nzima na siku ya kwanza ya mazoezi katika toleo la jana, leo tunakuletea na mambo yalivyokuwa siku ya pili na ya tatu yaani Jumapili na Jumatatu tukiangalia kazi ya kocha mpya wa makipa, Daniel Cadena Ledesma.
NI NANI HUYU
Ni mzaliwa wa kisiwa cha Baleares huko Mallorca nchini Hispania. Alizaliwa Januari 3, 1978 na ni msomi wa mpira mwezi leseni ya Uefa Pro ambayo ndiyo kubwa zaidi barani Ulaya. Ameshafanya kazi nchini Hispania katika klabu za Sevilla, Real Betis na Recreativo Huelva pamoja na China kwenye klabu za Guangzhou Mingtu na Shanghai Jiading. Cadena ana maarifa ya kutosha.
TIZI LAKE SASA
Katika siku za kwanza za mazoezi yake kocha huyo alianza na kutengeneza machale (instinct) kwa makipa. Ahmed Salula na Wilbol Maseke ni makipa wa Azam FC waliobaki ambao walicheza mechi nyingi msimu uliopita sambamba na Mathias Kigonya ambaye ameondoka.
Cadena anawekeza nguvu nyingi kwa hawa pamoja na Zubery Foba aliyepandishwa timu kubwa tangu msimu uliopita, lakini hakupata nafasi hata katika mechi moja.
Cadena anasema anaona uwezo mkubwa ndani ya makipa wake, lakini wanakosa maarifa sahihi ya kufundishwa.
Anaongeza kwamba kipa mpya Ali Ahamada atasaidia sana katika kuboresha uwezo wa makipa hawa kutokana na uzoefu wake. Kwa kawaida mazoezi huanza saa mbili asubuhi saa za Misri (sawa na saa tatu Tanzania).
Lakini, Cadena binafsi huanza saa moja kamili akiwa na Mwalo Ilunga ambaye amemchukua kama msaidizi wake kutoka timu za vijana Azam. Huwa naye uwanjani mapema asubuhi akimfundisha mbinu mbalimbali za kiufundi kama sehemu ya kumuandaa kuwa msaidizi mwenye viwango anavyotaka.
JUMAPILI
Hii ni siku ambayo Caden aliitumia zaidi kuwafundisha makipa namna ya kuusoma mchezo na kunusa hatari. Aliwachorea mistari katika maeneo mbali ya uwanjani na kuwataka wasogee sehemu fulani kila wakati mpira ukiwa kwenye mstari fulani.
Mpira ukiwa katikati ya uwanja, Cadena anawaambia makipa wake waanze kuchukua tahadhari.
Walifanya mazoezi haya kwa nusu saa nzima wakikimbia kwenda mbele na kurudi nyuma kila mara mpira ukihamishwa kutoka mstari mmoja kwenda mwingine.
Hii ilifanyika kwanza bila mpira kupigwa wala mchezaji kuwa na mpira. Ilihusu makipa wenyewe kusogea na kurudi, kusogea na kurudi.
Baada ya hapo ndipo yakaanza mazoezi ya kuwa na mpira halisi unaopigwa, lakini kwa kufuata mistari ileile. Ilifanyika hivi kwa dakika 15 na makipa walionekana kubadilika na kuanza kujua pa kukaa kutokana na sehemu ulipo mpira.
Baada ya hapo ndipo yakaja mazingira ya mchezo halisi wakiwepo washambuliaji na walinzi.
Cadena anasema haya ni mazoezi ya awali, lakini inamlazimu afanye kwa sababu anahisi waliyakosa katika hatua fulani ya makuzi yao kisoka.
JUMATATU
Siku iliyofuata, Jumatatu, ambayo ni ya tatu kambini, Cadena aliweka nguvu kuwaelekeza makipa kukabili hatari ya mmoja dhidi ya mmoja. Anasema kwenye mchezo kuna wakati kipa hubaki na mshambuliaji uso kwa uso.
Katika hali kama hiyo kuna maarifa ambayo kipa anatakiwa kuwa nayo ili kumkabili mshambuliaji kupunguza uwezekanao wa kuruhusu bao. Anasema amegundua makipa wake wanayo maarifa ya kukabiliana na hiyo hali uwanjani, lakini siyo ya kufundishwa - ni ya asili. Lazima kuwaongezea maarifa ili yakichanganyika na yale waliyonayo uwezo uongezeke.
Anatolea mfano Ahamada anavyoweza kukabiliana na hiyo hali.
Anasema kipa huyo amepitia mafunzo sahihi wakati sahihi na anajua vitu vingi, hivyo anaamini atamsaidia kuwaboresha Wengine. Alhamisi, Julai 27, Azam FC itacheza mechi ya kirafiki na Wadi Degla, timu ya Daraja la Kwanza ambayo imeshuka kutoka Ligi Kuu Misri msimu uliopita.