Shilla arejea Sweden kumalizia msimu
Muktasari:
- Msimu wa 2024/25 alifunga mabao 12 na asisti tano katika mechi 22 huku msimu wa 2023/24, akiwa U-17 akifunga mabao 15 na kutwaa tuzo ya MVP.
KIUNGO mshambuliaji wa AIK ya Sweden, Mohamed Shilla amerejea nchini humo baada ya kumaliza majukumu yake ya timu ya taifa ya Tanzania ya U-23, ambayo ilishindwa kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana hao (AFCON U-23) baada ya kutolewa na Kenya kwa jumla ya mabao 5-4.
Shilla alikuwa miongoni mwa wachezaji walioitwa katika kikosi cha U-23 chini ya Kocha Ahmad Ally, kilichokuwa na jukumu la kupambana na Kenya katika mechi mbili za kuwania tiketi ya kufuzu mashindano hayo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Shilla amesema kurejea kwake Sweden ni sehemu ya kuendelea na majukumu yake ya klabu baada ya kumaliza wajibu wa kuitumikia nchi.
Kiungo huyo alieleza anatarajia kukaa Sweden kwa takribani wiki tatu kabla ya kurejea tena Tanzania kwa ajili ya likizo.
“Kule kuna mambo nakwenda kuyaweka sawa natarajia kukaa kama wiki tatu ndio nitarudi tena Bongo kwa ajili ya likizo, tunapambana kama unavyofahamu unapocheza ligi kama ya Sweden lazima uishie ki profesheni hivyo lazima uendane na ratiba utakayopewa.”
Kiungo huyo alisajiliwa na AIK msimu uliopita baada ya kuonyesha kiwango bora katika ligi ya vijana msimu wa 2025/26 akiwa na Azam alifunga mabao nane na asisti tano kwenye mechi 14 akitwaa tuzo ya mchezaji bora wa ligi hiyo huku chama hilo likibeba ubingwa wa U-20.
Msimu wa 2024/25 alifunga mabao 12 na asisti tano katika mechi 22 huku msimu wa 2023/24, akiwa U-17 akifunga mabao 15 na kutwaa tuzo ya MVP.
Kiwango hicho alichokionyesha kiliwavutia mabosi hao na kumsajili na msimu uliopita nyota huyo alifunga mabao 12 na asisti saba.